Rais wa Kenya William Ruto siku ya Ijumaa amesema serikali itapunguza bei ya dizeli katika taifa hilo la Afrika Mashariki ili kuleta ahuweni kwa watu baada ya maandamano kuhusu kuongezeka kwa bei ya nishati kutokana na mapigano Mashariki ya Kati.
Wahudumu wa usafiri wa umma waliandamana mapema wiki hii kwa siku mbili. Watu wanne waliuawa katika maandamano hayo na wengine karibu 30 kujeruhiwa.
Katika hotuba kupitia televisheni, Ruto amesema kuwa ameagiza bei ya dizeli ipunguzwe kwa shilingi 10 kwa lita (dola 0.0772) katika mzunguko wa bei wa mwezi Juni na Julai, ili kuleta ahuweni kwa wananchi.
"Kupitia mpango wa serikali kwa serikali, tumepata hakikisho la kupata mafuta, licha ya kutatizwa kwa usambazaji, kuhakikisha tunapata mafuta kote nchini," Ruto amesema.
Amesema serikali imetumia kiasi kisichopungua shilingi bilioni 28.1 (zaidi ya dola milioni 216) katika hatua za kupunguza bei ya mafuta ikiwemo kuondoa kodi kati ya mwezi Aprili na Juni.
















