Kesi iliyokuwa ikimkabili mshukiwa mkuu wa mauaji ya kimbari ya Rwanda, Félicien Kabuga imefutwa rasmi kwenye Mahakama ya Kimataifa ya Uendeshaji wa Kesi Zilizobaki za Mahakama za Jinai (MICT).
Kulingana na taarifa iliyotolewa na MICT, Mei 20, 2026, uamuzi huo umefikiwa kufuatia kifo cha Kabuga, kilichotokea Mei 16, 2026 jijini The Hague nchini Uholanzi.
Kifo chake kilitokea wakati kesi yake katika Mahakama ya Kimataifa ya Uendeshaji wa Kazi za Masalia ya Mahakama za Uhalifu (MICT) ikiwa imesimama tangu mwaka 2023, baada ya madaktari kubaini kuwa hakuwa na uwezo wa kiafya kusimama kizimbani.
Kabuga alikuwa anakabiliwa na mashtaka matano mazito yaliyohusisha mauaji ya kimbari, kula njama za kutekeleza mauaji, na uhalifu dhidi ya ubinadamu, ambapo alituhumiwa kufadhili na kuongoza wanamgambo wa Interahamwe.
Baada ya kusakwa kwa miaka 26, alikamatwa nchini Ufaransa mnamo Mei 2020 na kuhamishiwa kwenye mahakama ya The Hague baadaye mwaka huo. Kesi yake ilianza kusikilizwa rasmi mnamo Septemba 2022.
Mahakama ya MICT ilipewa jukumu la kurithi kazi za Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu wa Rwanda (ICTR) na Yugoslavia ya zamani, baada ya kukamilisha rasmi shughuli zake nchini Tanzania.















