Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi, ameonya kwamba vikosi vya kigeni vinavyofanya operesheni karibu na Iran yakuwa “vinakabiliwa na hatari,” na kuvitaka kuondoka katika eneo hilo.
Kauli hiyo ilitolewa saa chache baada ya Rais wa Marekani, Donald Trump, kuahidi kujibu kile alichodai kuwa ni shambulio la Iran dhidi ya helikopta ya kijeshi ya Marekani.
Katika taarifa aliyochapisha kwenye mtandao wa X siku ya Jumanne, Araghchi alisema kuwa Mlango-Bahari wa Hormuz ni njia ya bahari inayoshirikiwa na Iran na Oman, na iko mbali na eneo la Marekani.
“Vikosi vyetu vyenye nguvu vya ulinzi viko katika hali ya tahadhari ya kudumu dhidi ya ukiukaji wowote wa anga, ardhi au maji ya Iran,” alisema.
Araghchi alionya kuwa majeshi ya kigeni yanayofanya shughuli karibu na Iran yanakabiliwa na hatari zinazoweza kusababishwa na “makosa ya kibinadamu, ajali za kawaida, au hata kujikuta katikati ya mapigano.”
“Ili kupunguza hatari, suluhisho bora ni kwa majeshi ya kigeni kuondoka haraka iwezekanavyo katika mazingira ambayo kamwe hayatakuwa rafiki kwa uwepo wa nguvu za uhasama,” aliongeza.
Mwanadiplomasia huyo mkuu alisema Iran inapendelea kutumia njia ya diplomasia, lakini akaonya kuwa Iran ina uwezo wa kujibu kwa mbinu nyingine iwapo itahitajika.
“Iran inapendelea lugha ya diplomasia. Hata hivyo, kama mashujaa wetu jasiri walivyoonyesha dunia, tunajua pia kuzungumza lugha nyingine,” alisema.
Kauli hizi zilikuja baada ya Trump kusema kwamba Marekani “lazima” ijibu kile alichodai kuwa ni shambulio la Iran lililosababisha kuanguka kwa helikopta ya kijeshi ya Marekani aina ya AH-64 Apache katika Mlango-Bahari wa Hormuz.
“Nimejulishwa na jeshi letu kuu kwamba usiku uliopita Wairani waliidungua moja ya helikopta zetu za kisasa aina ya Apache wakati ikifanya doria juu ya Mlango wa Hormuz,” Trump aliandika kwenye mtandao wake wa kijamii wa Truth Social.
Alisema marubani wote wawili waliokolewa bila kujeruhiwa, huku Kamandi Kuu ya Marekani baadaye ikithibitisha kuwa wafanyakazi wawili waliokuwa ndani ya helikopta hiyo waliokolewa baada ya ajali hiyo. Hata hivyo, kamandi hiyo ilisema chanzo cha tukio hilo bado kinachunguzwa.
Kauli hizi zinakuja wakati mvutano mpya ukiendelea katika eneo hilo kufuatia siku kadhaa za mapambano ya kijeshi yaliyohusisha Iran na Israel, licha ya juhudi za kidiplomasia zinazoendelea za kuhifadhi usitishaji mapigano ambao bado ni dhaifu.
















