Mkutano huo wa Kimataifa unawakutanisha pia wataalamu wa nishati, wawekezaji na mashirika ya kimataifa, ambapo utajadili matumizi ya nishati ya nyuklia kwa maendeleo ya barani Afrika.
Akihutubia mkutano huo, Rais Samia amesifu mchango wa Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki (IAEA) hasa katika kuunga mkono nchi za Kiafrika.
Rais Samia amesisitiza umuhimu wa kujengea umma uelewa ili kuondoa hofu ya matumizi ya nyuklia
"Nchi za Kiafrika sharti zielewe fursa na majukumu yanayohusiana na nishati ya nyuklia na maendeleo yake," amesema Rais Samia na kuongeza, "Uwazi, usalama na ulinzi wa mazingira na utawala unaowajibika bado inabaki kuwa vipaumbele muhimu katika mpango wa matumizi ya nyuklia.
Mkutano huo pia unalenga kujadili namna bora ya kuongeza upatikanaji wa nishati ya umeme Afrika, kupunguza uchafuzi wa mazingira, kusaidia maendeleo ya viwanda, kukuza ubunifu wa teknolojia za nishati ya nyuklia pamoja na kuvutia wawekezaji katika miradi ya nishati.
Wakati huo huo, Rais Samia amekutana na Mkurugenzi wa Shirika la Kimataifa la Nishati la Atomiki (IAEA), Rafael Mariano Grossi mara baada ya kumaliza mazungumzo pembezoni mwa Mkutano huo.














