Raia wanne wa Kenya wamefariki dunia na takriban wengine 30 wamejeruhiwa Jumatatu katika mgomo wa usafiri wa umma wenye lengo la kupinga kupanda kwa bei ya mafuta nchini humo.
Mgomo huo umetatiza kwa asilimia kubwa shughuli za kila siku hasa katika miji mikubwa kama vile Nairobi, Mombasa, Kisumu na kuendelea.
Bei ya mafuta imeshuhudiwa kupanda katika miezi ya hivi karibuni kufuatia mgogoro wa Mashariki ya Kati baada ya Mlango Bahari wa Hormuz ambao ndio njia kuu ya usafirishaji mafuta ghafi duniani kufugwa.
Kenya ni miongoni mwa nchi ambazo zimeathirika kwa kiasi kikubwa kutokana na utegemezi wake wa mafuta ghafi kutoka nchi za Ghuba.
Wiki iliyopita, serikali ya Kenya ilitangaza ongezeko la bei ya mafuta kufuatia kupanda kwa bei ya bidhaa hiyo katika soko la dunia, ikiwemo ongezeko la asilimia 23.5 kwa mafuta ya dezeli, hivyo kusababisha watoaji huduma wa usafiri wa umma kuitisha mgomo.
“Inasikitisha kwamba tumepoteza Wakenya wanne katika vurugu za leo, ambapo pia watu 30 wamejeruhiwa," amesema Waziri wa Mambo ya Ndani Kipchumba Murkomen.
Waziri Murkomen amedai kuwa, kuna baadhi ya magenge ya uhalifu yanayotumika kusababisha vurugu na kulenga mali za serikali na watu binafsi.
"Polisi pia imekamata watu 348 na baadhi ya vizuizi vilivyowekwa awali barabarani vimeondolewa," amesema.














