Hali ya taharuki imeweza kushuhudiwa katika baadhi ya barabara kuu nhcini Kenya baada ya usafiri kutatizika kutokana na mgomo wa matatu.
Usafiri ulikwama katika barabara kuu ya Nairobi–Namanga na kadhalika katika barabara kuu ya kuelekea Thika jijini Nairobi.
Mitaa kadha ya Kaunti ya Nairobi vile vile inashuhudia hali ya mshike mshike kati ya wanaopinga kupanda kwa bei ya mafuta na jeshi la polisi iliyosababisha kufungwa kwa barabara na kutatiza usafiri kwa jumla.
Aidha, barabara kuu ya Nairobi-Namanga ilifungwa na vijana waliokuwa wamekusanyika huku wengine wakichoma matairi katika eneo la Kitengela, kaunti ya Kajiado, mapema Jumatatu asubuhi.
Madereva wengi walilazimika kuepuka kutumia barabara hiyo, huku waliokuwa wakisafiri kutoka Nairobi kuelekea Kajiado na wale waliokuwa wakitoka Kajiado kuelekea Nairobi wakiegesha magari yao kando ya barabara.
Hali hiyo ilisababisha biashara nyingi kufungwa katika mji wa Kitengela, huku vijana wasiokuwa na shughuli wakimiminika mjini humo.
Mapema asubuhi, abiria wengi walikwama mjini humo baada ya magari ya usafiri wa umma kusitisha huduma kufuatia mgomo huo wa kitaifa.
Baadhi ya abiria walilazimika kutumia huduma za bodaboda na tuk-tuk, ambazo pia zilipandisha nauli zao.
Hata hivyo serikali ya Kenya imesema kuwa kupanda kwa mafuta imechochewa na mzozo unaondelea katika Mashariki ya Kati kufuatia kufungwa kwa Mlango-Bahari wa Hormuz, njia muhimu inayotumiwa kupatishwa kwa takriban asilimia 30 ya mafuta duniani.












