Bahrain imeweka zuio la mwezi mzima la kuingia wageni wanaotokea Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Sudan Kusini na Uganda, kwa hofu ya ugonjwa wa Ebola.
Marufuku hiyo inakuja wakati mataifa hayo matatu yakiwa yameathirika kwa kiasi kikubwa na ugonjwa huo ambao hadi kufikia sasa, umegharimu maisha ya watu zaidi ya 130.
"Tumesitisha uingiaji wa raia kutoka Sudan Kusini, DRC na Uganda kuanzia leo,” ilisema sehemu ya taarifa ya Mamlaka ya Usalama wa Anga ya Bahrain.
"Uamuzi huu unatokana na taarifa za hivi karibuni kuhusu kuenea kwa ugonjwa huu kwenye nchi tajwa."
Siku ya Jumanne, Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani, iliwatahadharisha raia wake kuhusu kutembelea nchi zilizoathirika zaidi na ugonjwa wa Ebola.
Kuenea kwa kasi kwa ugonjwa huo, pia umelilazimu Shirika la Afya Duniani (WHO) kuelezea wasiwasi wake, likitadhaharisha kuwa, huenda ugonjwa huo ukasambaa kwa muda mrefu.















