Somalia imepokea vifaa vya kisasa kutoka Shirika la Ushirikiano na Uratibu la Uturuki TIKA siku ya Jumapili kwa lengo la kuboresha na kusasisha shughuli za kilimo katika Wizara ya Kilimo na Umwagiliaji.
Msaada wa Uturuki utasaidia ufanisi wa taasisi, kuharakisha upatikanaji wa huduma na kusaidia Somalia kuwa na chakula cha uhakika, amesema Waziri wa Kilimo wa Somalia Mohamed Abdi Hayir Mareye katika taarifa yake.
“Napenda kuishukuru TIKA, taasisi ya maendeleo ya taifa la ndugu zetu, Jamhuri ya Uturuki, kwa kuwasilisha msaada wa awamu ya kwanza," amesema Waziri katika sherehe ya makabidhiano iliyofanyika katika mji mkuu wa Mogadishu.
Amesema ombi liliwasilishwa kwa rais wa TIKA Abdullahi Eren katika mkutano uliofanyika Ankara mwaka 2025.
'Tunathamini ushirikiano huu'
Vifaa vya msaada vilivyowasilishwa ni pamoja na kompyuta, printa na televisheni.
“Tunathamini sana ushirikiano huu na tunategemea kuendelea kushirikiana na marafiki zetu wa Uturuki," amesema.
Somalia na Uturuki wamekuza ushirikiano wao kuanzia mwaka 2011 baada ya Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan (wakati huo waziri mkuu) alipoitembelea nchi hiyo.
Tangu wakati huo, msaada wa kibinadamu nchini Somalia umefikia kiasi cha Dola bilioni 1, ikiwemo miradi katika sekta ya afya, elimu, huduma za manispaa, na miundombinu.
















