Mamlaka za taifa la Kaskazini magharibi la Mauritania zinasema kuwa wahamiaji haramu zaidi ya 500 wameokolewa katika bahari yao katika kipindi cha siku 10 zilizopita.
Katika operesheni ya hivi karibuni, vikosi vya wanamaji vya Mauritania vimewaokoa wahamiaji 77 kwa kuizuia mashua yao kwenye bahari yao, kulingana na taarifa iliotolewa na Wizara ya Uvuvi Alhamisi.
Wizara inasema boti hiyo ilikuwa imetoka Conakry, mji mkuu wa nchi jirani ya Guinea, na ilikuwa imebeba wanaume 59, wanawake 11, na watoto saba, wote raia wa Guinea.
Mamlaka zinasema mashua hiyo iliondoka pwani ya Guinea usiku wa Mei 29 kabla ya kuonekana na maafisa wa doria wa Mauritania.
Juhudi za uokoaji
Operesheni ya sasa imeongeza idadi ya wahamiaji waliookolewa Mauritania katika kipindi cha siku 10 zilizopita kufikia 503, kufuatia shughuli mbali mbali za uokoaji zilizoongozwa na vikosi vya wanamaji.
Wahamiaji haramu kutoka Kusini mwa Jangwa la Sahara wanajaribu safari hiyo hatari kupitia visiwa vya Hispania vya Canary.


















