Waziri Mkuu wa Tanzania Mwigulu Nchemba amewataka viongozi nchini humo kuwaelimisha wananchi kuhusu umuhimu wa kuandikishana mikataba pindi wanapopeana ardhi badala ya kufanya hivyo kwa kuaminiana.
"Viongozi mliopo hapa waambieni wananchi hivi sasa masuala ya ardhi wasifanye kwa kuaminiana, wawe wanaandikishana kwa mikataba na tena katika ofisi za kijiji ili watambulike," amesema.
Kauli hiyo ametoa Juni 7, 2026 alipokuwa akizungumza na viongozi wa kada mbalimbali wa mkoa wa Iringa katika kikao cha majumuisho ya ziara zake.
"Ninawasihi wananchi tusiogope kurasimisha mambo yetu kwa sababu uaminifu unapungua. Tunaporasmisha, tunaepusha migogoro siku za usoni," amesisitiza.
Ushauri huo umetolewa kufuatia kuongezeka kwa wimbi la migogoro katika sekta ya ardhi.
Wakati huo huo, amewataka viongozi wanapotaka kufanya uendelezaji wowote nao pia wahakikishe wanawapa wananchi husika mikataba ili kulinda haki yao.
"Tusichukue maeneo ya watu bila kuwalipa fidia. Kama kuna uendelezaji ni lazima kuwe na mikataba rasmi. Wananchi wa eneo husika wapewe barua za kuonesha utwaaji huo wakati wakisubiri fedha za fidia zipatikane. Liwe ni eneo limetengwa kwa uwekezaji, ujenzi wa barabara au shule, watu wapewe barua. Ardhi ni jambo rasmi ndiyo sababu presha ya matumizi inazidi kuongezeka," alisema.

















