Watu wasiopungua 49 wamefariki kwa kiu baada ya gari lao kuharibika na kukwama kwa siku kadhaa katika Jangwa la Sahara kaskazini mwa Niger, mamlaka zimesema.
Waliofariki wote ni raia wa Niger, ambao walikuwa wanarudi nyumbani kutoka katika hafla ya dini nchini Mali wakati gari lao lilipokwama wakiwa zaidi ya kilomita 80 magharibi mwa Assamaka, karibu na mipaka ya Mali na Algeria, ofisi ya gavana wa kanda ya Agadez nchini Niger alisema katika ujumbe wa mtandao wa kijamii siku ya Alhamisi.
Watu wawili walinusurika baada ya kutembea kwa zaidi ya kilomita 50 walipopata maji na kuendelea na safari yao hadi Assamaka, walipofahamisha mamlaka, ofisi hiyo ya gavana imesema.
Ujumbe uliotumwa katika eneo hilo na Gavana wa Agadez Jenerali Ibra Boulama Issa umebaini kuwa gari hilo lilisafiri kwa siku kadhaa kutoka mji wa Mali wa Talhandek karibu kilomita 300 kutoka mpaka wa Niger.
Haikufahamika mara moja chanzo cha kuharibika kwa gari na kama abiria walikuwepo eneo hilo kwa muda gani.
Wote 49 walizikwa kwenye makaburi la pamoja eneo hilo kwa kile maafisa wamekitaja kuwa “hali mbaya na ya kuchosha” kwa walionusurika.



















