Mahakama ya Mali imeamuru kifungo cha miaka 20 jela dhidi ya afisa katika ubalozi wa Ufaransa anayetuhumiwa kuwa jasusi kwa lengo la "kudhoofisha usalama wa taifa".
Akiwa amezuiliwa tangu kukamatwa kwake Agosti 2025, Mfaransa huyo pia alipigwa faini ya euro 5,400 ($6,225) na kupigwa marufuku kwa miaka 20 kuingia Mali.
Wakati wa kukamatwa kwake, mamlaka ya Mali ilimshutumu afisa huyo, aliyetambulika kama Yann V., kwa kufanya kazi katika idara ya kijasusi ya Ufaransa, na kuwatukana "mataifa ya kigeni" yaliyokuwa yanajaribu kuyumbisha nchi.
Alizuiliwa Agosti 13 akiwa na maafisa kadhaa wa Mali, wanaodaiwa kupanga mapinduzi nchini humo.
Ufaransa ilisisitiza tena kwamba mashtaka dhidi ya afisa huyo, ambaye alikuwa akifanya kazi katika ubalozi wa Ufaransa katika mji mkuu, Bamako, hayana mashiko.
"Wakala wetu amehusishwa katika kesi za kisheria zinazohusisha tuhuma zisizo na msingi," wizara ya mambo ya nje ya Ufaransa ilisema Ijumaa.
"Afisa wetu alikuwa akitekeleza ujumbe wa ushirikiano wa kiusalama na kwa vyovyote vile Ufaransa haijashiriki, moja kwa moja au kwa njia isiyo ya moja kwa moja, katika kuivuruga Mali."



















