Timu ya taifa ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo imesitisha mazoezi kwa ajili ya fainali za Kombe la Dunia yaliyopangwa kufanyika nyumbani baada ya taifa hilo kukumbwa na mlipuko wa Ebola, afisa wa timu hiyo ameiambia AFP Jumatano.
Mlipuko huo wa homa kali inayoambukiza ulitangazwa mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo Ijumaa iliopita.
Mlipuko huo ambao umetokea kwa mara ya 17 nchini DRC tayari unashukiwa kusababisha vifo vya watu 139 na wengine 600 kuambukizwa.
Kambi ya mazoezi ambayo ilikuwa ianze mjini Kinshasa kwa siku tatu "imepelekwa Ubelgiji," afisa wa mawasiliano wa timu ameiambia AFP, bila kusema iwapo mlipuko wa Ebola ndio sababu ya mabadiliko hayo.
‘Hakuna wachezaji wa ndani’
"Hakuna wachezaji wa ndani ya nchi waliochaguliwa" katika kikosi cha taifa, ameongeza.
DRC imefuzu kushiriki fainali za Kombe la Dunia, ambalo litafanyika nchini Marekani, Mexico na Canada, kwa mara ya pili baada ya kucheza mara ya kwanza 1974, wakati nchi hiyo ikijulikana kama Zaire.
Wamepanga kuweka kambi Houston wakati wa michuano, ambapo watacheza katika kundi K na mechi ya kwanza ikiwa Juni 17 dhidi ya Ureno.
Timu hiyo baadae imeratibiwa kwenda Guadalajara nchini Mexico kucheza na Colombia Juni 24 na kisha kurudi Atlanta, Marekani ambapo watavaana na Uzbekistan Juni 28.
Kulegezwa kwa masharti ya kusafiri
Afisa wa serikali ya Marekani amesema Jumanne kuwa timu hiyo itaruhusiwa kusafiri na kucheza katika Kombe la Dunia.
Marekani imepiga marufuku raia wasio wa Marekani ambao wamekuwa nchini DRC, Uganda na Sudan Kusini katika siku 21 zilizopita kuingia nchini humo kutokana na mlipuko wa Ebola.
Marekani inasema, timu ya DRC tayari ilikuwa inafanya mazoezi Ulaya, hivyo haihusiki na marufuku hayo.
Lakini wangekuwa nchini DR Congo ndani ya siku 21, hivyo wangelazimika kufanyiwa vipimo ambavyo vinafanyiwa raia wa Marekani-lakini sio katazo la moja kwa moja.















