Kamandi ya Marekani inayohusika na Afrika imesema imefanya mashambulizi ya ziada ya anga dhidi ya magaidi kaskazini mashariki mwa Nigeria siku ya Jumapili, katika operesheni iliyofanyika kwa ushirikiano na serikali ya Nigeria.
AFRICOM ilithibitisha siku ya Jumatatu kwamba hakuna wanajeshi wa Marekani wala wa Nigeria waliojeruhiwa katika mashambulizi hayo.
Haya yanajiri baada ya operesheni nyingine ya pamoja iliyofanyika siku ya Jumamosi, ambapo majeshi ya Marekani na Nigeria yalifanikiwa kumuua Abu-Bilal al-Minuki, aliyekuwa kiongozi mwandamizi wa kundi la kigaidi la Daesh (ISIS) katika eneo hilo la kaskazini mashariki mwa Nigeria.
Rais wa Marekani Donald Trump na Rais wa Nigeria Bola Ahmed Tinubu walithibitisha tukio hilo, wakieleza kuwa operesheni hiyo ilikuwa ni hatua muhimu katika mapambano dhidi ya ugaidi.
Rais Tinubu alisema majeshi ya Nigeria yalishirikiana kwa karibu na jeshi la Marekani katika kile alichokiita “operesheni ya ujasiri ya pamoja” iliyokuwa pigo kubwa mtandao wa magaidi nchini humo.
Kwa upande wake, Rais Trump aliishukuru serikali ya Nigeria kwa ushirikiano wake katika operesheni hiyo, akisema ni hatua muhimu katika juhudi za kupambana na ugaidi. Hata hivyo, hapo awali Trump aliwahi kuishutumu Nigeria kwa kushindwa kuwalinda Wakristo dhidi ya mashambulizi ya magaidi.
Nigeria kwa sasa inapambana na makundi kadhaa, yakiwemo matawi ya kikanda ya Daesh na kundi la Boko Haram. Pia inakabiliana na magenge ya wahalifu wanaojulikana kama “bandits”, ambao hujihusisha na utekaji nyara kwa ajili ya fidia.
Kwa mujibu wa taarifa, Marekani pia imepeleka mamia ya wanajeshi nchini Nigeria katika siku za hivi karibuni ili kutoa mafunzo na kuimarisha uwezo wa majeshi ya nchi hiyo, baada kuongezeka kwa mvutano kati ya mataifa hayo mawili.













