| Swahili
AFRIKA
2 dk kusoma
Mgomo wa usafiri wa umma Kenya kuhusu kupanda kwa bei ya mafuta wasitishwa
Mgomo huo wa wahudumu wa usafiri wa umma umesitishwa kwa wiki moja baada ya maandamano ya siku mbili yaliyosababisha vifo vya watu wanne.
Mgomo wa usafiri wa umma Kenya kuhusu kupanda kwa bei ya mafuta wasitishwa
Waandamanaji wakiweka vizuizi barabarani wakati wa maandamano ya wahudumu wa usafiri wa umma. / Reuters

Wahudumu wa usafiri wa umma nchini Kenya siku ya Jumanne walisitisha mgomo wa nchi nzima kwa wiki moja kutoa nafasi kwa majadiliano na serikali, kuashiria kumalizika kwa siku mbili za maandamano yaliyosababisha watu wanne kuuawa na zaidi ya 30 kujeruhiwa.

Mazungumzo yalitibuka siku ya Jumatatu wakati wahudumu wa usafiri walipotaka bei ya mafuta ipunguzwe ili kuwapunguzia wao na abiria gharama ya nauli.

Abiria walikwama kwa siku ya pili mfululizo Jumanne huku wahudumu wa usafiri wa umma wakiwa wamezuia magari yao yasifanye kazi.

Waandamanaji walijitokeza barabarani, na kukabiliana na polisi pamoja na kuchoma moto matairi.

Bei ya mafuta nchini Kenya ilipanda zaidi siku ya Ijumaa, huku dizeli ikiongezeka kwa asilimia 23.5. Serikali imetaja sababu kuwa ni kutokana na vita vya Iran na athari yake kwa upatikanaji wa nishati.

Waziri wa Mambo ya ndani Kipchumba Murkomen, amesema majadiliano na wadau wote wa sekta ya mafuta yatafanyika katika siku saba zijazo kuangalia suala la bei.

Mwakilishi wa wahudumu wa usafiri, Kennedy Kaunda, amesema wanachama watatoa nafasi kwa majadiliano kuendelea, na kama hakutakuwa na muafaka, umma utapewa maelekezo katika kipindi cha wiki moja.

Watu wanne waliuawa Jumatatu na zaidi ya 30 kujeruhiwa. Watu 348 pia walikamatwa na watafikishwa mahakamani kwa mashtaka ya kufanya mgomo usio halali.

CHANZO:TRT Afrika Swahili