| Swahili
Maoni
AFRIKA
4 dk kusoma
Jukwaa la Kidiplomasia la Antalya kwa mtazamo wa viongozi wa Afrika
Antalya ndiyo sehemu ambayo nchi zinazoendelea zimepata sauti sasa.
Jukwaa la Kidiplomasia la Antalya kwa mtazamo wa viongozi wa Afrika
Viongozi kadhaa wa Afrika walifanya mazungumzo na Rais wa Uturuki Recep Tayip Erdogan katika Jukwaa la Kidiplomasia la Antalya 2025. / TRT Global

Na Adem Koç

Kwa miaka mingi, Jukwaa la Kidiplomasia la Antalya limeibuka kuwa zaidi ya jukwaa la kuwasilisha dira ya sera ya mambo ya nje ya Uturuki. Limekuwa jukwaa la kidiplomasia ambalo viongozi wa Afrika wanaweza kueleza maono yao wakati mtazamo wa dunia unapobadilika.

Kuwepo kwa viongozi wengi kutoka bara la Afrika 2026 ni dhihirisho kuwa mabadiliko haya siyo sadfa. Antalya siyo tu sehemu ya mikutano; ni eneo la kimkakati ambapo Afrika inabadilisha muelekeo wake katika dunia ambayo mambo yanachukua mkondo mwingine.

Kwa kutazama kwa makini ujumbe wa viongozi wa Afrika jijini Antalya kuna masuala matatu yanayojirudia; Umiliki wa kikanda, mfumo wa kusambaza uwezo kote duniani, na kuimarisha ushirikiano wa kimkakati katika ngazi ya taasisi na Uturuki.

Kwanza, msisitizo wa umiliki wa kikanda ni muhimu. Hotuba iliotolewa Antalya na Rais wa Burundi Evariste Ndayishimiye, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika, ilisisitiza dhamira ya Afrika kutoka kuwa bara linalosubiri misaada ya nje na kutafuta suluhu ya matatizo yao wenyewe.

Mtazamo huu unasaidia kueleza sera ya Uturuki kwa bara zima la Afrika. Uturuki kujihusisha siyo eti kunaonekana kama kufanya maamuzi kwa niaba ya Afrika, lakini kama kuunga mkono Afrika kitaasisi na uhuru wa kimkakati.

Uwepo wa Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo Félix Tshisekedi katika jukwaa hilo pia kulidhihirisha upanuzi wa sera ya Uturuki kuhusu Afrika.

Kwa miaka mingi, kujihusisha kwa Uturuki na Afrika kwa sehemu kubwa kulionekana kupitia shughuli zake Mashariki na Kaskazini mwa Afrika.

Mikutano ya Antalya imeonesha kuwa Uturuki sasa inaonekana zaidi katika maeneo ya usalama wa Afrika ya Kati, usimamizi wa rasilimali, na ujumuishaji wa kikanda. Hili linaonesha kufikia kwa Uturuki katika sera yake ya Afrika ya hatua ya pili, ambayo ni pana zaidi.

Hivyo hivyo, msisitizo wa Rais wa Somalia Hassan Sheikh Mohamud kuhusu diplomasia ulibaini mfumo thabiti zaidi wa ushirikiano kati ya Uturuki na Afrika. Katika suala la Somalia, Uturuki haionekani tu kama muwekezaji au mshirika katika misaada, lakini kama mchangiaji mkubwa wa kuimarisha taasisi za serikali.

Mtazamo huu unasaidia kueleza kwa nini viongozi wengi wa Afrika wanaendelea kuiona Uturuki kama mshirika “tofauti”. Ujumbe uliotolewa Antalya ulidhihirisha namna uhusiano huu wa kuaminiana sasa hivi unaimarishwa kitaasisi katika kazi ya kidiplomasia.

Ushirikiano ‘tofauti’

Ushirikiano katika masuala ya usalama ulijadiliwa kwa kina kwenye jukwaa hilo ambao ulikuwa muhimu kwa Afrika. Mafanikio katika maeneo kama mafunzo kwa vikosi maalum na ushirikiano wa teknolojia ya ulinzi kati ya Uturuki na Nigeria yalidhihirisha kuwa Antalya siyo sehemu ya mazungumzo tu—ni jukwaa ambalo ushirikiano wa kimkakati unaundwa.

Licha ya kuwepo kwa tofauti kati ya Uturuki na Uganda kuhusu masuala ya Somalia, uwakilishi wa ngazi ya juu wa Uganda katika mkutano wa Antalya ulionesha kuwa ushirikiano wa Uturuki na mataifa ya Afrika uko kitaasisi zaidi.

Kwa mantiki hii, Antalya siyo tu jukwaa la kuanzisha ushirikiano mpya, bali la kuimarisha ushirikiano uliopo kwa sasa.

Kupanua wigo wa kidiplomasia

Moja ya masuala muhimu yaliyojitokeza kwenye jukwaa hilo kwa mtazamo wa Afrika ni matarajio kuhusu uwezo wa upatanisho wa Uturuki. Ukizingatia mizozo kama ya Sudan, mvutano kati ya Somalia na Ethiopia, ukosefu wa usalama katika eneo la Sahel, na changamoto zilizokithiri za usalama Afrika ya Kati, kupanua wigo wa kidiplomasia wa Uturuki kupitia majukwaa kama Antalya inatarajiwa kuwa na nafasi muhimu zaidi katika miaka ijayo.

Ujumbe uliowasilishwa na viongozi wa Afrika katika jukwaa hilo bila shaka unaonesha imani kwa uwezo wa Uturuki kuchangia katika usalama wa kikanda.

Kwa Afrika, Jukwaa la Kidiplomasia la Antalya linaonesha kuwa ni zaidi ya kongamano. Limekuwa fursa ambayo bara la Afrika linajieleza katika mfumo wa kimataifa, jukwaa ambalo ushirikiano unaundwa, na sehemu ya kujadili misingi ya kitaasisi.

Katika mchakato huu, Uturuki siyo tu iko katika nafasi ya mwenyeji; inaendelea kuwa mshirika mwenza katika kuongoza mijadala ulimwenguni —ambapo bara la Afrika halishiriki likiwa pembeni, bali likiwa sehemu ya mjadala wenyewe.

Mwandishi, Adem Koç Mhadhiri, Chuo Kikuu cha Nairobi.

CHANZO:TRT Afrika