Sehemu kadhaa za mji mkuu wa Libya, Tripoli, zimeshuhudia maandamano kuanzia Jumapili hadi Jumatatu kutokana na kuzorota kwa huduma za kijamii, vyombo vya habari nchini humo vimeripoti.
Waandamanaji wamelalamikia tatizo la kukatika kwa umeme na maji mara kwa mara, huduma mbovu za afya na kupanda kwa gharama za maisha, kwa mujibu wa Shirika la Habari la Libya-LANA.
Waandamanaji walichoma moto matairi ya magari katika maeneo ya Tajoura, Souq al-Jumaa, Al-Sarraj, Janzour, Zawiyat al-Dahmani na Al-Dhahra na kufunga barabara, imesema LANA.
Pia waliweka vizuizi katika taasisi za umma, ikiwemo Wizara ya Mambo ya Nje na Televisheni ya Taifa katika eneo la Zawiyat al-Dahmani.
Serikali ya Umoja wa Kitaifa, inayoongozwa na Abdulhamid Dbeibeh, imekuwa madarakani tangu 2021 kukabiliana na tatizo la umeme, ambalo lilipata utatuzi kati ya mwaka 2023 na 2025.
Libya bado imegawanyika kati ya serikali mbili hasimu: serikali ya Umoja wa Kitaifa inayotambulika kimataifa, inayoongozwa na Dbeibeh iliyopo mjini Tripoli, ambayo inaongoza magharibi mwa nchi, na serikali iliyochaguliwa na Baraza la Wawakilishi mapema 2022, hivi sasa ikiongozwa na Osama Hammad ikiwa na makao makuu Benghazi, ambayo inatawala eneo la mashariki na sehemu kubwa ya kusini.
Kwa miaka mingi, Misheni ya Umoja wa Mataifa nchini Libya imetaka kutatua tatizo la uongozi nchini humo kuelekea uchaguzi, ambapo raia wengi wa Libya wana imani kwamba unaweza kumaliza mgogoro ambao umedumu tangu kuondolewa kwa Muammar Gaddafi mwaka 2011.


















