Raia wawili wa Ghana wamewasilisha ombi kwa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) kuitaka ianzishe uchunguzi kuhusu mashambulizi dhidi ya raia wa kigeni nchini Afrika Kusini, wakisema kuwa vitendo hivyo vinaweza kufikia kiwango cha uhalifu dhidi ya ubinadamu.
Afrika Kusini imekumbwa na ongezeko la maandamano ya kupinga wahamiaji katika miezi ya hivi karibuni, huku baadhi ya maandamano hayo yakihusishwa na vurugu dhidi ya wageni. Waandamanaji wamekuwa wakiwalaumu wahamiaji kwa baadhi ya matatizo kama uhalifu na ukosefu wa ajira.
Ombi hilo, ambalo limeonekana na shirika la habari Reuters na kuwasilishwa mahakamani tarehe 15 Julai, linadai kuwepo kwa "mtindo wa mashambulizi yaliyoenea na ya kimfumo" dhidi ya wahamiaji nchini Afrika Kusini. Pia linaishutumu serikali ya Rais Cyril Ramaphosa kwa kushindwa kuzuia au kuwaadhibu wahusika wa uhalifu huo, ikiwemo uhalifu wa mauaji.
Ombi hilo liliwasilishwa na Palgrave Boakye-Danquah, aliyekuwa msemaji wa zamani wa serikali ya Ghana kuhusu masuala ya utawala na usalama, pamoja na Emmanuel Kotin, mchambuzi wa masuala ya ugaidi na usalama.
"Kwa miaka mingi, ndugu na dada zetu Waafrika wamekuwa wakiuawa, kupigwa na kufukuzwa kutoka kwenye makazi yao nchini Afrika Kusini," walisema katika taarifa kwa vyombo vya habari.
Taarifa hiyo iliongeza: "Ingawa tunawapongeza baadhi ya watu nchini Afrika Kusini ambao wamekemea vitendo hivi, ukubwa, kiwango na kujirudia kwa vurugu hizi kunazua maswali mazito kuhusu kushindwa kwa mamlaka za serikali kuzuia, kuchunguza na kuwaadhibu wahusika wa uhalifu huu."
Msemaji wa Rais Ramaphosa hakujibu mara moja ombi la kutoa maoni kuhusu suala hilo. Awali, Ramaphosa amekuwa akilaani mashambulizi hayo na kuonya dhidi ya kuwalaumu wahamiaji kwa matatizo ya muda mrefu yaliyopo nchini.
Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Afrika Kusini alikataa kutoa maoni kuhusu ombi hilo. ICC, ambayo hushughulikia mashtaka ya uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinadamu, pia haikutoa ufafanuzi wowote kuhusi ombi hilo.
Wahamiaji kadhaa kutoka nchi za Afrika wameuawa katika vurugu hizo, huku wengine wakipigwa na kushuhudia nyumba na maduka yao yakiporwa. Maelfu ya wengine wamekimbia nchi hiyo.
Afrika Kusini imekuwa ikishuhudia matukio ya vurugu za chuki dhidi ya wageni kwa miaka kadhaa, licha ya kuwa idadi ya wahamiaji wanaoishi nchini humo — takriban asilimia 5 ya jumla ya watu wake — ni ndogo ikilinganishwa na viwango vya kimataifa.









