Wizara ya Masuala ya Dini ya Kiislamu nchini Somalia itaanza mpango wa kitaifa wa kusajili misikiti, shule zinazofundisha Qur'an na viongozi wa dini kama sehemu ya jitihada za kudumisha uangalizi wa taasisi za dini, ametangaza Waziri Sheikh Mukhtaar Robow Ali.
Tangazo hilo limefuatia mkutano na mkurugenzi mkuu wa wizara na wakuu wa vitengo kutathmini maendeleo ya mabadiliko ya kitaasisi na vipaombele vya serikali.
Waziri ameamuru kuanza mara moja kwa usajili utakaohusisha misikiti na shule za Qur'an.
Usajili huo utakapokamilika, wizara ina mpango wa kutoa mafunzo kuongeza elimu na stadi kwa maimamu wa misikiti na vyuo vilivyosajiliwa.
Mafunzo
Mpango huo ni sehemu ya mabadiliko mapana yenye lengo la kuwa na takwimu rasmi za taasisi za dini na viongozi wake, huku ikiunga mkono jitihada za serikali za kuweka katika viwango sawa vya elimu ya dini na kudumisha ushirikiano na viongozi.
Robow alisifu uongozi wa wizara kwa kuharakisha mabadiliko na kuboresha uwajibikaji wa ndani, na kusema hatua hiyo imeboresha uratibu na kusaidia kufufua miradi ambayo awali ilikuwa nyuma ya ratiba.
Tanganza hilo linakuja wakati Somalia inajiandaa na mahafali ya kwanza kutoka taasisi ya masomo ya dini mwishoni mwa wiki hii, na kuwa hatua kubwa katika jitihada za wizara katika kupanua elimu rasmi ya Kiislamu.
Robow aliwataka wakurugenzi wa idara kufanya kazi kwa karibu na uongozi wa wizara kuboresha huduma kwa umma na kuhakikisha mipango ya serikali inatekelezwa kwa ufanisi.













