| Swahili
ULIMWENGU
4 dk kusoma
‘King of the North’ Burnham achukua uongozi wa chama cha Labour, aahidi kuiunganisha Uingereza
Andy Burnham ameahidi kuongeza ujenzi wa nyumba za umma ili kusaidia kutatua tatizo la ukosefu wa makazi na kuongeza rasilimali katika huduma za ustawi wa jamii.
‘King of the North’ Burnham achukua uongozi wa chama cha Labour, aahidi kuiunganisha Uingereza
Burnham aahidi kufufua matumaini akiwa Waziri Mkuu ajaye wa Uingereza. / / AFP

Andy Burnham ameahidi "kuwarejeshea matumaini" wananchi wa Uingereza baada ya kuthibitishwa kuwa kiongozi mpya wa Chama tawala cha Labour, hatua ambayo inamfungulia njia ya kuwa Waziri Mkuu mpya wa Uingereza.

"Kwa muda mrefu sana, watu na maeneo mbalimbali yamesubiri siasa kuwarudishia matumaini. Sisi tutawarejeshea matumaini hayo," alisema katika mkutano maalumu wa chama.

"Mimi ni kwa ajili yetu, kwa ajili ya wote," aliwaambia wajumbe waliokuwa wakimshangilia siku ya Ijumaa.

Burnham anamrithi Keir Starmer, aliyejiuzulu mwezi uliopita kama Waziri Mkuu baada ya miezi kadhaa ya misukosuko ya kisiasa.

Chama cha Labour, chenye mrengo wa kushoto wa wastani, bado kinaendelea kuwa na chama cha wengi bungeni baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2024. Hivyo, kiongozi wa chama hicho kikubwa zaidi ndiye anayekuwa Waziri Mkuu bila kufanyika uchaguzi mpya.

Ni wiki nne tu zimepita tangu Burnham, aliyekuwa meya wa Manchester, aliporejea bungeni kwa kishindo baada ya kutokuwapo kwa miaka tisa, akiwa na dhamira ya kumrithi Starmer.

Siku ya Jumatatu atakuwa Waziri Mkuu wa saba wa Uingereza ndani ya kipindi cha miaka kumi.

Wabunge wa Labour wanaamini Burnham ndiye mwenye nafasi nzuri zaidi ya kukabiliana na Chama cha Reform UK kinachoongozwa na Nigel Farage, chenye msimamo mkali dhidi ya wahamiaji na kinachohusishwa na mrengo wa kulia wenye misimamo mikali. Tafiti za maoni zinaonyesha Reform UK kinaweza kushinda uchaguzi mkuu ujao unaotarajiwa kufanyika mwaka 2029.

"Ofisi ya Number 10 North"

Burnham, anayejulikana kwa jina la utani “King of the North” (Mfalme wa Kaskazini) kutokana na kushinda uchaguzi wa umeya wa Greater Manchester mara tatu mfululizo, anaamini katika kugawa zaidi madaraka kwa miji mingine ili kuchochea uchumi wa Uingereza.

Miongoni mwa mapendekezo yake ni kuanzisha ofisi ya "Number 10 North", sawa na makao ya Waziri Mkuu yaliyopo eneo la Downing Street lakini kwa upande wa kaskazini mwa nchi.

Alisema kuwa katika kipindi cha miongo minne iliyopita, tangu miaka ya 1980, maeneo yaliyojenga msingi wa Chama cha Labour pamoja na jamii za vijijini na maeneo ya pwani nchini Uingereza hayakutendewa haki.

"Ndiyo maana leo tunawaahidi kwamba tutafanya vizuri zaidi."

"Ikiwa tunataka uchumi na taifa vinavyowanufaisha watu wote na maeneo yote, basi tunahitaji kufuata njia mpya tofauti na ile tuliyoifuata kwa miaka 40 iliyopita," alisema.

Burnham, anayehesabiwa kuwa mmoja wanaofuata mrengo wa kushoto wa wastani ndani ya Labour, anaunga mkono kuongezwa kwa usimamizi wa serikali katika huduma muhimu pamoja na kufufua sekta za viwanda.

Baada ya kutopata mpinzani yeyote, amekuwa kiongozi wa Labour katika jaribio lake la tatu, baada ya kushindwa katika uchaguzi wa uongozi wa chama mwaka 2010 na 2015.

Kiongozi mpya

Burnham ameahidi kuongeza ujenzi wa nyumba za umma ili kusaidia kupunguza tatizo la ukosefu wa makazi na kuongeza fedha kwa huduma za ustawi wa jamii.

Starmer alikiwezesha Labour kurejea madarakani mwezi Julai 2024 baada ya miaka 14 ya kuwa upinzani, kwa ushindi mkubwa dhidi ya Chama cha Conservative, ambacho kilibadilisha mawaziri wakuu watano kutokana na misukosuko iliyotokana na kura ya maoni ya Brexit ya mwaka 2016.

Hata hivyo, uongozi wa Starmer ulianza kukumbwa haraka na changamoto mbalimbali za sera za ndani pamoja na mabishano, ikiwemo kumteua Peter Mandelson, aliyewahi kuhusishwa na Jeffrey Epstein, kuwa balozi wa Uingereza nchini Marekani.

Matokeo mabaya ya uchaguzi wa serikali za mitaa na wa kikanda mwezi Mei yaliongeza shinikizo dhidi ya Starmer. Shinikizo hilo liliongezeka zaidi baada ya Burnham kushinda uchaguzi mdogo wa ubunge tarehe 18 Juni, jambo lililomruhusu kugombea uongozi wa chama.

Changamoto zilezile za zamani

Burnham, ambaye mara nyingi huonekana akiwa amevaa fulana nyeusi na koti, ameungwa mkono na wabunge 379 kati ya 403 wa Labour. Hakuna aliyefanikiwa kupata idadi ya kura za uteuzi 81 zilizohitajika ili kumpinga.

Hata hivyo, atakabiliwa na changamoto zilezile zilizomkabili Starmer, ikiwemo uchumi unaokua kwa kasi ndogo, gharama kubwa za serikali kukopa, pamoja na ongezeko la wahamiaji wanaoingia nchini kwa njia zisizo rasmi kupitia boti ndogo, hali ambayo imeongeza uungwaji mkono kwa chama cha Reform UK.

Aidha, kupanda na kushuka kwa bei za nishati kutokana na vita vya Marekani dhidi ya Iran kunaweza pia kuathiri utawala wake.

Burnham ataapishwa rasmi kuanza kazi siku ya Jumatatu baada ya kukutana na Mfalme wa Uingereza, Mfalme Charles III. Ameahidi kuendelea kutekeleza ahadi za Ilani ya Uchaguzi ya Labour ya mwaka 2024, ikiwemo kutoongeza kodi kuu za nchi.

Hata hivyo, atalazimika kutafuta vyanzo vingine vya fedha ili kuziba pengo la takribani Dola bilioni 6.3 ndani ya miaka minne katika mpango wa uwekezaji wa sekta ya ulinzi, pamoja na kushughulikia suala tata la mageuzi ya mfumo wa ustawi wa jamii.

 

CHANZO:AFP