Mkuu wa Mawasiliano wa Uturuki, Burhanettin Duran, amesema kuwa jaribio la mapinduzi lililoshindwa la tarehe 15 Julai 2016 lilikuwa tukio la kihistoria lililobadili mwelekeo wa taifa hilo, huku akizitaka nchi washirika kuunga mkono juhudi za Uturuki dhidi ya kundi la FETO, akilieleza kuwa ni tishio linalovuka mipaka ya nchi ya Uturuki.
Duran alitoa kauli hiyo Jumanne, akisema kuwa matukio ya Julai 15 yameunda mustakabali wa taifa hilo.
"Usiku wa tarehe 15 Julai 2016 ulikuwa usiku uliounda mustakabali wa taifa letu kwa kila namna. Ushindi wa usiku huo unatokana na msimamo thabiti na wa kujitegemea wa kisiasa wa Rais Recep Tayyip Erdogan pamoja na uongozi wake tangu dakika za mwanzo kabisa," alisema Duran katika ujumbe wa video uliowasilishwa kwenye kongamano la kuadhimisha miaka 10 tangu jaribio hilo la mapinduzi lililoshindwa.
Alisema kuwa wakati wa jaribio hilo, wanachama wa kundi la FETO walishambulia taasisi za serikali, bunge na vyombo vya habari, huku wananchi wa Uturuki wakijitokeza kwa wingi mitaani kufuatia wito wa Rais Erdoğan.
Kwa mujibu wa Duran, watu 253 walipoteza maisha na maelfu wengine walijeruhiwa katika matukio hayo.
Aliongeza kuwa Uturuki imefanikiwa kuondoa ushawishi wa FETO ndani ya taasisi za serikali, lakini imebeba gharama kubwa kufanya hivyo.
"Tumepitia nyakati ngumu na zenye changamoto nyingi. Lakini, hata iwe vigumu kiasi gani, Uturuki chini ya uongozi wa Recep Tayyip Erdogan ina uwezo wa kukabiliana na vitisho vya aina hii vinavyolenga uhuru na mamlaka ya taifa letu," alisema.
Duran pia alizitaka nchi washirika wa Uturuki kuunga mkono juhudi za nchi hio dhidi ya kundi hilo.
"Tunatarajia marafiki zetu kusimama nasi na kuonyesha mshikamano dhidi ya miundo inayolenga uhuru na demokrasia ya taifa letu. FETO si suala la usalama wa kitaifa la Uturuki pekee; ni tishio la wazi kwa kila nchi ambamo linaendesha shughuli zake," alisema.
Aidha, Duran alisema kuwa jaribio hilo la mapinduzi lilionyesha namna mashirika ya kigaidi na vitisho vya aina mbalimbali vinavyofanya kazi kwa njia tata, akisisitiza kuwa nchi zinazokabiliwa na changamoto kama hizo zinapaswa kushirikiana ili kupata suluhisho la pamoja kwa matatizo ya usalama yanayoikabili dunia.


















