Rais wa Marekani Donald Trump amesema kuwa huenda Marekani ikachukua jukumu la kusimamia na kulinda Mlango-Bahari wa Hormuz, na inapaswa kulipwa kwa kufanya hivyo kutokana na umuhimu wa njia hiyo katika usafirishaji wa nishati duniani.
"Tutaudhibiti mlango huo wa bahari, na huenda tukausimamia. Tutakuwa walinzi wa Mlango wa Hormuz. Labda tutajiita 'walinzi wakuu wa Mlango huo wa Bahari.' Na tunapaswa kulipwa kwa kufanya hivyo," Trump alisema katika mahojiano ya simu na Shirika la Habari la Fox News siku ya Jumatatu.
Aliongeza kuwa Marekani inapaswa kulipwa kwa gharama za kuhakikisha usalama wa njia hiyo.
"Tutailinda. Tutalipwa kwa kuilinda — fedha nyingi," alisema Trump.
Alisema mataifa mengine yanayonufaika na usalama wa Mlango wa Hormuz yana uwezo mkubwa wa kifedha na yanapaswa kuchangia gharama hizo.
"Tutarejeshewa gharama hizo, kwa sababu mataifa mengine ni tajiri sana. Yako upande wetu, na hatuwezi kutarajiwa kufanya kazi hiyo bure," alisema.
Trump: "Tutawashambulia kwa nguvu"
Kauli ya Trump imekuja wakati mvutano kati ya Marekani na Iran ukiongezeka kuhusu udhibiti wa Mlango wa Bahari wa Hormuz, njia muhimu inayopitisha sehemu kubwa ya mafuta yanayosafirishwa duniani.
Baada ya kutangaza kufungwa kwa njia hiyo siku ya Jumamosi kufuatia kile ilichodai kuwa ni kupita njia hio bila ruhusa, Iran ilisema siku ya Jumapili kuwa usafirishaji utabaki kusitishwa hadi hali ya utulivu na usalama itakaporejea.
Trump alisema kuwa makubaliano yaliyokuwa yamefikiwa na Iran yalivunjwa.
"Tulikuwa na makubaliano. Yalikuwa yamekamilika, lakini wakayavunja. Wao huvunja kila mara. Tumekuwa na makubaliano 10 nao, hivyo sasa tutawashambulia kwa nguvu kubwa," alisema.
Iran yaonya kuhusu kuingilia kati kwa Marekani
Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Iran (IRGC) lilisema katika taarifa yake siku ya Jumatatu kuwa njia pekee ya kurejesha usafiri wa kawaida kupitia Mlango wa Hormuz ni kusitishwa kwa operesheni za kijeshi za Marekani katika eneo hilo.
Iran ilionya kuwa kuendelea kwa kile ilichokiita kuingiliwa kwa uendeshaji wa Hormuz kunaweza kusababisha matukio makubwa zaidi katika sekta ya mafuta na gesi duniani.
Majeshi ya Marekani na Iran zilishambuliana kwa makombora na ndege zisizo na rubani mwishoni mwa wiki na hadi Jumatatu.
Iran ilidai kuwa imeshambulia vituo vya kijeshi vya Marekani katika eneo la Ghuba na kuendelea kuufunga Mlango wa Hormuz, hatua iliyosababisha bei ya mafuta kupanda katika masoko ya kimataifa.
Mabadiliko hayo yanaashiria ongezeko kubwa la mashambulizi katika eneo hilo katika wiki iliyopita, huku yakitia mashaka makubaliano ya muda kati ya Marekani na Iran yaliyolenga kufungua tena mlango huo na kusitisha mapigano wakati pande hizo zikiendelea na mazungumzo ya siku 60.

















