Jeshi la Marekani limeanzisha mashambulizi dhidi ya Iran kwa usiku wa tano mfululizo, kwa mujibu wa taarifa ya jeshi hilo.
Mashambulizi hayo, yaliyoanza saa 12:00 jioni kwa saa za GMT, yalifanyika kwa lengo la kuendelea kudhoofisha uwezo wa kijeshi wa Iran, kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kamandi Kuu ya Jeshi la Marekani (CENTCOM) kupitia mtandao wa X.
Msemaji wa Ikulu ya White House, Karoline Leavitt, alisema mapema kwamba sababu ya mashambulizi ya hivi karibuni ya Marekani ni kwamba Iran ilikiuka makubaliano ya maelewano yaliyokuwa yamefikiwa kati ya pande hizo.
"Haswa, katika makubaliano hayo ya maelewano waliyotia saini, walikubaliana kutoshambulia meli za kibiashara zinazopita katika Mlango wa Bahari wa Hormuz. Kwa bahati mbaya, wamechukua uamuzi wa kusikitisha wa kukiuka makubaliano kwa kufanya mashambulizi hayo," alisema.
Shambulio la Marekani karibu na hospitali ya kutibu watoto wenye saratani
Iran imelaani shambulio la Marekani lililofanyika karibu na hospitali ya kutibu watoto wenye saratani katika mji wa Ahvaz, kusini-magharibi mwa nchi hiyo, ikilitaja kuwa ni “shambulio la kikatili”.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Esmaeil Baqaei, alisema Hospitali ya Shahid Baqaei, kituo maalumu cha kutibu watoto wenye saratani, ilihamisha wagonjwa wake usiku wa Jumatano baada ya shambulio la Marekani.
“Wale wanaoendelea kuhubiri kuhusu haki za binadamu, lakini kwa makusudi wanafumbia macho mashambulizi dhidi ya hospitali na vituo vya afya, wamepoteza kabisa hadhi ya kimaadili,” alisema msemaji huyo.















