| Swahili
AFRIKA
2 dk kusoma
Wanafunzi 20 wafariki katika ajali ya basi la shule Uganda
Nchi hiyo ya Afrika Mashariki ina rekodi mbaya ya usalama wa barabarani, mara nyingi kukiripotiwa ajali za mabasi ya abiria na magari ya mizigo.
Wanafunzi 20 wafariki katika ajali ya basi la shule Uganda
Baadhi ya watu wengine, wakiwemo wafanyakazi wa shule, walijeruhiwa katika ajali hiyo.

Basi lililokuwa na wanafunzi wanaokuwa wakitoka ziara ya masomo lilipoteza muelekeo nchini Uganda, na kusababisha vifo vya watoto 20, na mtu mzima mmoja, kwa mujibu wa ripoti ya polisi ya Ijumaa.

Nchi hiyo ya Afrika Mashariki ina rekodi mbaya ya usalama barabarani, mara nyingi kukiripotiwa ajali za mabasi ya abiria na magari ya mizigo.

"Kwa masikitiko, watoto 20 na mtu mzima mmoja, ambaye ndie mkurugenzi, Bwana Tadeo Ssekade, wamefariki," Waziri wa Serikali za Mitaa, Balaam Ateenyi Barugahara, ameandika katika mtandao wa X alipokuwa katika eneo la ajali.

Basi hilo kutoka Shule ya King David Junior iliyopo jijini Kampala, lilikuwa linarudi kutoka safari ya mafunzo kutoka eneo la Maporomoko ya Sipi katika wilaya ya Kapchorwa pindi lilipopoteza muelekeo na kuacha njia, kwa mujibu wa uchunguzi wa polisi wa awali.

Vifo

"Inaarifiwa kwamba, dereva alipoteza muelekeo, na kugonga jiwe kubwa pembezoni mwa barabara, na basi kupinduka," polisi imesema katika taarifa yake kupitia mtandao wa X.

"Ajali hiyo imesababisha vifo vya watoto 20 na mtu mzima mmoja, huku watu wazima watatu na watoto kadhaa wakijeruhiwa," imeongeza taarifa hiyo.

Polisi ilionesha picha ya basi lililopinduka na kuharibika, na kusema uchunguzi unaendelea, huku waliojeruhiwa wakiendelea kupata matibabu hospitalini.

“Tumekuta watoto 9 wakiwa katika hali mbaya,” amesema Waziri Barugahara kupitia X.

Ajali za mabasi ya abiria zinatokea mara kwa mara nchini Uganda.

Mwezi Oktoba, mabasi mawaili yaligongana katika barabara kuu, na kuuwa takriban watu 46.

Ripoti ya mwaka 2024 inasema kuna ajali mbaya 4,434 na vifo 5,144 mwaka huo.