| Swahili
ULIMWENGU
3 dk kusoma
Nigeria yawaua magaidi wa Daesh, yaokoa mateka saba katika operesheni za kijeshi
Vikosi vya usalama pia vilizuia jaribio la magaidi wanaoshukiwa kuwa wa Daesh la kutega vilipuzi katika barabara.
Nigeria yawaua magaidi wa Daesh, yaokoa mateka saba katika operesheni za kijeshi
Wanajeshi pia walipata silaha, risasi na vitu vingine katika operesheni hizo zilizoratibiwa. / / AFP

Wanajeshi wa Nigeria wamefanya operesheni za kiusalama nchini humo ikiwemo kuwaokoa watu saba waliokuwa wametekwa nyara. Wanajeshi hao pia wamewaua magaidi wawili wanaohusishwa na Daesh, na kuwakamata wengine wanne katika operesheni za pamoja zilizofanyika katika majimbo ya Borno, Yobe, Benue na Plateau, kwa mujibu wa Shirika la Habari la Nigeria (NAN).

Operesheni hiyo, iliyopewa jina la "Operation Hadin Kai", iliwaokoa wanawake wawili na watoto wawili waliotoroka kutoka maficho ya Daesh katika eneo la Agapalawa, lililopo kwenye Milima ya Mandara Wilaya ya Gwoza, Jimbo la Borno.

Ripoti hiyo iliongeza kuwa mwanamke mmoja na mtoto wake, wanaoaminika kuwa ndugu wa mpiganaji wa Daesh, pia walijisalimisha kwa wanajeshi baada ya kutoroka kutoka maficho ya Gobara katika Msitu wa Sambisa.

Katika operesheni tofauti zilizofanywa kwa ushirikiano na Civilian Joint Task Force (CJTF), wanajeshi waliwakamata watu wanne wanaoshukiwa kuwa magaidi wa Daesh pamoja na washirika wao katika wilaya za Gwoza, Gujba na Kukawa zilizoko katika majimbo ya Borno na Yobe.

Magaidi walilazimika kurudi nyuma

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, mmoja wa washukiwa alikiri kuwa alikuwa akiwapeleleza wanajeshi waliokuwa wakifanya operesheni za kusafisha eneo kwenye barabara ya Baga–Cross Kauwa na kuwapatia kundi hilo la kigaidi msaada wa vifaa na huduma za kiutendaji.

Vikosi vya usalama pia vilizuia jaribio la magaidi wanaoshukiwa kuwa wa Daesh kuingia katika eneo la Kirawa, wilayani Gwoza, na kuwafanya warudi nyuma. Ripoti hiyo ilisema kuwa baadaye ndege ya Jeshi la Anga la Nigeria ilimuua mshukiwa mwingine wa ugaidi.

Katika tukio jingine jimboni Borno, wanajeshi waligundua na kuliharibu bomu la (IED) lililokuwa limetegwa kando ya barabara kuu ya Maiduguri–Gamboru katika Wilaya ya Dikwa, hivyo kuzuia kile ambacho mamlaka zilisema kingeweza kuwa shambulio dhidi ya watumiaji wa barabara hiyo.

Katika Jimbo la Benue, wanajeshi waliokuwa chini ya "Operation Whirl Stroke", wakisaidiwa na wawindaji wa jadi pamoja na Kikosi cha Ulinzi wa Raia cha Jimbo la Benue, waliwaokoa watu wanne waliotekwa nyara na kuwaua washukiwa wawili wa utekaji nyara wakati wa operesheni za kuyaondoa na kudhibiti magaidi.

Silaha na vifaa vyakamatwa

Operesheni hiyo pia ilisababisha kukamatwa kwa bunduki moja aina ya AK-47, bunduki moja aina ya G3, bastola moja, risasi 221 za aina mbalimbali, bunduki, sare za kijeshi za kuficha utambulisho (camouflage), pamoja na mashine ya malipo ya kielektroniki (POS) kutoka maficho ya washukiwa.

Ripoti hiyo iliongeza kuwa wanajeshi waliwakamata watu watano wanaoshukiwa kuwa wanachama wa makundi ya kigaidi katika msako uliofuatia kwenye maficho ya wahalifu katika Wilaya ya Otukpo, Jimbo la Benue.

Aidha, wanajeshi walikamata mapipa 15 ya petroli iliyokuwa ikisafirishwa kwa njia ya magendo, huku kikosi cha Operation Delta Safe kikibomoa eneo la kusafishia mafuta ghafi kinyume cha sheria na kukamata vifaa vinavyodaiwa kutumika katika wizi wa mafuta ghafi katika Jimbo la Rivers.

 

CHANZO:TRT Afrika and agencies