Rais wa Misri, Abdel Fattah El-Sisi amewasili nchini Tanzania Julai 18, 2026 kwa ziara ya kitaifa na kupokelewa na mwenyeji wake Rais Samia Suluhu Hassan.
Wakati huo huo, Rais El-Sisi alikagua gwaride rasmi la mapokezi lililoandaliwa na Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) katika viwanja vya Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Ziara hiyo ni sehemu ya jitihada pana za kudumisha ushirikiano kati ya Misri na Tanzania.
Rais El-Sisi na mwenyeji wake Rais Samia Suluhu Hassan wanatarajiwa kufanya mazungumzo yatakayolenga kuimarisha uhusiano wa kihistoria kati ya mataifa hayo mawili, pamoja na kupanua ushirikiano katika sekta mbalimbali za maendeleo, ikiwemo biashara, uwekezaji, kilimo, nishati, maji, afya, elimu na miundombinu.
Ziara hiyo inaelezwa na wachambuzi wa masuala ya kiuchumi na diplomasia kuwa ni muhimu katika kudumisha ushirikiano wa kidiplomasia na kufungua ukurasa mpya wa ushirikiano.
Viongozi hao pia watashiriki katika Jukwaa la Biashara la Tanzania na Misri, litakalowakutanisha wafanyabiashara na wawekezaji kutoka nchi hizo mbili, kwa lengo la kujadili fursa za biashara na uwekezaji.
Mara ya mwisho kwa Rais El-Sisi kuitembelea Tanzania ilikuwa ni Agosti 17, 2017, ambapo alikutana na mwenyeji wake aliyekuwa Rais wa nchi hiyo wakati huo Hayati John Pombe Magufuli.
Mazungumzo yao yalijikita zaidi katika kuongeza ushirikiano wa kibiashara, na kukamilisha utiaji saini wa mikataba mikubwa ya miundombinu.
Itakumbukwa kuwa, baadhi ya makampuni ya Misri yanahusika katika ujenzi wa miundombinu mikubwa nchini Tanzania ikiwemo mradi wa uzalishaji umeme kutoka Bwawa la Mwalimu Nyerere wenye thamani ya Dola bilioni 2.9.















