Shirika la Afya Duniani (WHO) limesema Sudan bado ndiyo nchi inayokabiliwa na mgogoro mkubwa zaidi wa kibinadamu duniani, ambapo zaidi ya watu milioni 33 wanahitaji msaada wa kibinadamu.
Wizara ya Afya imetangaza siku ya Jumanne kuwa maambukzi yanayoshukiwa kuwa ya kipindupindu yameripotiwa katika majimbo manne, wakati ugonjwa huo ukiendelea kuenea sambamba na kuzorota kwa hali ya kibinadamu iliyosababishwa na vita vinavyoendelea.
Tangazo hilo lilitolewa mjini Khartoum, katika kituo cha Operesheni za Dharua ambapo maafisa wamejadili hali ya afya ya umma nchini, kwa mujibu wa taarifa ya wizara hiyo.
Wizara hio haikutoa idadi ya watu wanaoshukiwa kuambukizwa, lakini imethibitisha kuwa visa hivyo vimeripotiwa katika majimbo ya Kordofan Kaskazini, Kordofan Magharibi, Darfur Kusini na Khartoum.
Aidha, wizara hio ilisema maambukizi ya ugonjwa wa surua yamepungua, huku maambukizi mapya 25 yameripotiwa, bila ya kuwa na vifo vyovyote.
Mnamo Julai 10, Shirika la Afya Duniani (WHO) limeonya kuwa mlipuko wa kipindupindu unaendelea kuenea katika maeneo ya Darfur na Kordofan, baada ya kuripotiwa vifo 114 na maambukizi zaidi ya 1,330, likiongeza kuwa idadi hiyo huenda ikaongezeka.
WHO imeeleza kuwa Sudan ndiyo inayokabiliwa na mgogoro mkubwa zaidi wa kibinadamu duniani, ambapo zaidi ya watu milioni 33 wanahitaji msaada wa kibinadamu, wakiwemo milioni 21 wanaohitaji huduma za afya.
Shirika hilo pia limesema watu milioni 13.4 wamelazimika kuyahama makazi yao, kati yao milioni 9 wakiwa wamehama ndani ya Sudan na milioni 4.6 wakikimbilia nchi jirani.












