Mwenyekiti wa Baraza la Mpito la Sudan Abdel Fattah al-Burhan ametembelea miji ya Umm Sayala na Jabrat al-Sheikh katika jimbo la Kordofan Kaskazini Jumatatu, siku moja baada ya jeshi kuchukua udhibiti wa maeneo mawili kutoka kwa wapiganaji wa RSF.
Taarifa kutoka kwa baraza hilo inasema al-Burhan, ambaye pia ni mkuu wa majeshi, alikagua vikosi vilioko katika mstari wa mbele Umm Sayala na Jabrat al-Sheikh.
Alikuwa ameongozana na Gavana wa Darfur Minni Arko Minnawi, Gavana wa Kordofan Kaskazini Abdel Khaliq Abdel Latif na kamanda wa Vikosi vya Sudan Shield Abu Aqla Keikel.
Siku ya Jumapili, jeshi lilisema kuwa vikosi vyake vimechukua udhibiti wa miji ya Bara, Jabrat al-Sheikh na Umm Sayala kufuatia makabiliano na RSF. Miji miwili iko katika njia ya kimkakati inayounganisha Sudan ya kati na kanda za Kordofan kaskazini na Darfur magharibi.
Majimbo ya Kaskazini, Magharibi na Kusini yamekumbwa na mapigano makali kati ya jeshi la Sudan na RSF tangu Oktoba 2025.
Sudan imejikuta kwenye mapigano kati ya jeshi la RSF tangu Aprili 2023. Vita hivyo vimesababisha vifo vya maelfu ya watu na mamilioni wengine kuondolewa kwenye makazi yao.

















