| Swahili
UTURUKI
2 dk kusoma
Mwanadiplomasia mkuu wa Uturuki Fidan ajadili Cyprus, Syria na masuala ya kikanda na Guterres
Kupitia mazungumzo ya simu, pande zote mbili zilijikita katika masuala yanayojiri hivi sasa Mashariki ya Kati na Mashariki mwa Mediterenia.
Mwanadiplomasia mkuu wa Uturuki Fidan ajadili Cyprus, Syria na masuala ya kikanda na Guterres
Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki Hakan Fidan na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres wamejadili masuala ya kikanda.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki Hakan Fidan Jumapili alijadili masuala ya kikanda kwa njia ya simu na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres.

Kwa mujibu wa vyanzo vya kidiplomasia vya Uturuki, Fidan na Guterres wamejadili masuala ya kikanda yanayohusiana na ziara ya Katibu Mkuu nchini Syria na katika visiwa vya Cyprus.

Umoja wa Mataifa utawasilisha taarifa ya kina kwa Baraza la Usalama baadae mwezi huu kuhusu ukiukaji wa sheria unaofanywa na Israel nchini Syria, amesema Guterres.

Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari mjini Damascus, Guterres amehimiza kwamba ukiukwaji unaofanywa na Israel dhidi ya uhuru wa mipaka wa Syria "haukubaliki," na kuitaka Israel kufuata Makubaliano ya Kujiondoa ya mwaka 1974.

“Mauaji ambayo Syria imeshuhudia hayajawakatisha tamaa watu wa Syria katika kutafuta malengo yao halali," ameongeza.

Pia ameonya kuwa msaada wa kibinadamu wa Umoja wa Mataifa umefikia asilimia 20 pekee kwa mahitaji ya watu wa Syria.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amewasili Damascus Jumamosi kwa ziara ya siku tatu na kufanya mazungumzo na Rais Ahmed al Sharaa na Waziri wa Mambo ya Nje Asaad al Shaibani, ambapo pia alisisitiza dhamira ya Umoja wa Mataifa kwa uhuru wa Syria, heshima ya mipaka na kuitaka jumuia ya kimataifa kuiunga mkono baada ya machafuko.

Umoja wa Mataifa umetangaza siku ya Alhamisi kwamba Guterres atasafiri kuelekea Cyprus kuendeleza mchakato wa amani.

"Katibu Mkuu atasafiri kwenda Cyprus kuanzia tarehe 27 mpaka 29 Julai kama sehemu ya misheni ya ofisi yake na dhamira yake katika suala la Cyprus," amesema msemaji wake Stephane Dujarric katika mkutano na waandishi wa habari.

Amesema kuwa, Guterres atakutana na Rais wa Jamhuri ya Kituruki ya Kupro ya Kaskazini (TRNC) Tufan Erhurman na Nikos Christodoulides, kiongozi wa Cyprus ya Kusini iliyo chini ya Ugiri, Dujarric amesema Guterres pia atakutana na "wadau wengine na kujadili jitihada za kuendeleza mchakato wa amani na kuunga mkono utulivu katika kisiwa, ikiwemo kupitia kazi ya misheni ya amani ya Umoja wa Mataifa UNFICYP iliyopo."