Rais Yoweri Museveni wa Uganda amelazimika kuahirisha maadhimisho ya Siku ya Mashahidi wa Uganda kufuatia tishio la ugonjwa wa Ebola, unaoripitiwa kuanzia mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
Kulingana na Rais Museveni, uamuzi huo umefikiwa baada ya mashauriano na kikosi kazi cha kitaifa cha kudhibiti magonjwa ya mlipuko pamoja na viongozi wa dini, kutokana na hatari ya kusambaa kwa ugonjwa wa Ebola unaoendelea kuripotiwa Mashariki mwa DRC, ambako mahujaji wengi hutoka, kuelekea Uganda kila mwaka.
Museveni aliwataka mahujaji walioanza safari ya kuelekea nchini Uganda, kuanza kurudi makwao na kuchukua hatua stahiki za kujilinda dhidi ya ugonjwa huo.
Sherehe za mahujaji wa Uganda (Siku ya Mashahidi wa Uganda) ni maadhimisho ya kidini yanayofanyika kila Juni 3. Huwakumbuka na kuwaheshimu Wakristo 45 (Wakatoliki 22 na Waanglikana 23) waliouawa kati ya 1885 na 1887 na Mfalme Mwanga II wa Buganda kwa kukataa kukana imani yao.
Sherehe hizi hufanyika katika Madhabahu ya Namugongo, iliyoko umbali wa kilomita 15 kutoka mji mkuu wa Uganda, Kampala.
















