| Swahili
AFRIKA
1 dk kusoma
Uganda yakanusha madai ya Marekani ya kufadhili kliniki za Ebola nchini humo
Wizara ya afya ya Uganda inasema haina taarifa kuhusu pale vituo hivyo vya matibabu vilipo katika nchi yao.
Uganda yakanusha madai ya Marekani ya kufadhili kliniki za Ebola nchini humo
PICHA YA MAKTABA: Daktari nchini Uganda akijiandaa kumpa chanjo mtu aliyetangamana na mgonjwa wa Ebola. / Reuters

Wizara ya afya ya Uganda imekanusha madai ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani kuwa Marekani inafadhili ujenzi wa kliniki 50 katika maeneo yaliyoathiriwa na Ebola nchini humo.

Mlipuko ulipatikana mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo Ijumaa iliopita na unashukiwa kusababisha vifo vya watu 139 na maambukizi karibu 600.

Maambukizi mawili pia yamethibitishwa katika nchi jirani ya Uganda.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ametangaza Jumanne kuwa wameahidi kufadhili vituo 50 vya kutibu Ebola katika maeneo yaliyokumbwa na mlipuko huo nchini DRC na Uganda.

‘Hatuna taarifa hizo’

Lakini wizara ya afya ya Uganda ilisema siku ya Jumatano kuwa haijawahi kujadili kuhusu ujenzi wa vituo vya matibabu.

Katika taarifa, wizara ilisema "haina taarifa ya pale vituo hivyo vilipo nchini mwao".

“Tunaendelea kuthibitisha kuwa Uganda imebaini maambukizi mawili ya Ebola kutoka nje kufikia sasa: mtu mmoja amefariki na mwingine bado anatibiwa. Hakuna maambukizi ya ndani ya nchi na hali ni shwari kwa sasa,” taarifa ilisema.

Marekani imepiga marufuku raia wasiokuwa wa Marekani ambao wametoka DRC, Uganda au Sudan Kusini katika siku 21 zilizopita kuingia nchini kwao kutokana na mlipuko.

CHANZO:TRT Afrika