| Swahili
ULIMWENGU
1 dk kusoma
Trump na Netanyahu watofautiana kwa njia ya simu kuhusu kuishambulia Iran — Ripoti
Waziri Mkuu wa Israel anaripotiwa kuishinikiza Marekani kuishambulia Iran, huku Rais Trump akisisitiza kuwa kuna uwezekano wa kufikia makubaliano, kwa mujibu wa taarifa za vyombo vya habari.
Trump na Netanyahu watofautiana kwa njia ya simu kuhusu kuishambulia Iran — Ripoti
Vyombo vya habari vya Marekani vinaripoti kuwa Trump na Netanyahu wametofautiana kuhusu Iran. (Picha: MAKTABA) / AP

Rais wa Marekani Donald Trump na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu wametofautiana Jumanne kwa njia ya simu kuhusu namna ya kuendeleza mapigano nchini Iran, hayo ni kwa mujibu wa vyombo vya habari vya Marekani.

Mazungumzo hayo yalikuja baada ya Trump kumjulisha Netanyahu siku ya Jumapili kuhusu maandalizi ya kuanzisha tena mashambulizi mapya dhidi ya Iran, operesheni iliyotarajiwa kuitwa 'Operation Sledgehammer,' kwa mujibu wa taarifa ya awali ya CNN.

Hata hivyo, Trump baadae alitangaza kusitisha mpango wa mashambulizi yaliyopangwa kufanyika Jumanne kufuatia kile alichokiita ombi la kuahirisha mashambulizi kutoka mataifa washirika ya Ghuba, ikiwemo Qatar, Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu.

Nchi hizo zimekuwa katika majadiliano ya kina pamoja na maafisa wa Ikulu ya White House na Pakistan kuangalia ni jinsi gani wanaweza kufufua upya mazungumzo ya kidiplomasia, vimesema vyanzo vya karibu.

Katika mazungumzo ya simu ya muda mrefu yaliyofanyika Jumanne, Netanyahu amemuambia Trump kwamba kusitisha mashambulizi ilikuwa ni kosa kubwa na kumtaka kuendelea na mpango wa kuishambulia Iran kama ilivyopangwa awali, vimesema vyanzo vya Marekani na Israel.

“Tofauti ilikuwa wazi, Trump alitaka kuona iwapo makubaliano yangefikiwa, lakini Netanyahu alitarajia kitu chengine tofauti,” afisa mmoja kutoka Israel aliiambia CNN.