Wanaharakati wanaoiunga mkono Palestina wanapanga kuizunguka Ikulu ya Marekani wakati wa maandamano yao ya wikiendi hii.
Maandamano hayo yamepangwa kufanyika siku ya Jumamosi, kulingana na wanaharakati kutoka makundi ya CODEPINK na baraza la Uhusiano wa Kimarekani na Uislamu, miezi nane toka kuanza kwa mashambulizi katika eneo la Gaza yalioua makumi kwa maelfu ya Wapalestina na kusababisha hali mbaya ya kibinadamu na uharibifu mkubwa.
Marekani, ambaye ni mshirika mkubwa wa Israeli, imeshuhudia miezi mingi ya maandamano yenye kuiunga mkono Palestina, kupitia maandamano katika mji wa Washington na mikesha karibu na Ikulu ya Marekani, huku waandamanaji wakifunga barabara na madaraja.
Maofisa wapatao nane katika serikali ya Rais Joe Biden, tayari wamejiuzulu, kama ishara ya kupinga sera za kiongozi huyo. Waandamanaji hao pia wametatiza shughuli za kampeni za Rais Biden.
"Kama maandalizi ya matukio wikendi hii huko Washington, DC, ambako kuna uwezekano wa kuwepo umati mkubwa wa watu kukusanyika, hatua za ziada za usalama wa umma zimewekwa karibu na Ikulu ya Marekani," amesema msemaji kutoka idara ya intelijensia ya nchi hiyo.