Wapalestina wakikagua eneo la lililoshambuliwa na Israeli dhidi ya shule inayohifadhi watu waliokimbia makazi yao, katika Jiji la Gaza, Agosti 10, 2024. /Picha: Reuters

Na

Sundos Hammad

Mnamo mwaka wa 2000, nikiwa mtoto wa miaka tisa nikishuhudia Intifadha ya Pili, nilielewa uhusiano wa kina kati ya elimu na kuishi chini ya wanyakuzi wa ardhi.

Kila asubuhi, kwenda shule yangu ya msingi katika mji wa al-Bireh katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu, ilikuwa ni kitendo cha ukaidi.

Vifaru vya Israeli viliwekwa karibu na lango la shule yangu, na mwisho wa siku, watoto wadogo kama mimi walikuwa wakiwarushia mawe askari waliokuwa kwenye makazi ya karibu.

Askari walijibu kwa risasi za moto. Nikiwa na hofu niliporudi nyumbani, nilihoji kwa nini sisi kama watoto wa Kipalestina tulilazimika kustahimili hatari hizo za kila siku, lakini mama yangu alisisitiza kila mara: "Elimu si chaguo. Ni maisha yako ya baadaye, na mustakbali wa kizazi kijacho."

Leo, siku za usoni zinaonekena kuwa mbaya.

Kwa zaidi ya siku 335, zaidi ya Wapalestina milioni mbili wamenyimwa haki zao za kimsingi za kuishi huku kukiwa na mashambulizi ya Israeli.

Huku kukiwa na mauaji ya kimbari huko Gaza, wanafunzi kote ulimwenguni wanajiandaa kwa ajili ya kuanza kwa mwaka mpya wa masomo, mfumo wa elimu nchini Palestina umekuwa mhanga wa vita.

Shule za Gaza zimekuwa zikilengwa na kulipuliwa kwa mabomu, huku zikifanywa kuwa makazi ya watu waliokimbia makazi yao. Si hilo tu, katikati ya shida hii, begi la shule liligeuzwa kuwa begi la kujiokoa.

Nakumbuka nilitazama video fupi ya msichana huyu mdogo sana ambaye aliamua kubeba vitabu vyake kwenye begi alipokuwa akikimbia nyumbani kwao, akisema kwa sura nzuri: "Nimehifadhi vitabu vyangu."

Mwezi Mei mwaka huu, vyuo vikuu vya Gaza vilitoa taarifa kuthibitisha kuwepo kwao na azma ya pamoja ya kuanza tena kufundisha huko Gaza katika taasisi zao, licha ya uharibifu wa sekta ya elimu ya juu na vikosi vya Israeli.

Wakipinga kutokomezwa kwa elimu inayoendelea, walitangaza: "Tulijenga vyuo vikuu hivi kutumia mahema. Na tutaendelea kujenda shule kutokana na mahema kupitia msaada wa marafiki zetu."

Kulemazwa kwa elimu

Tangu Oktoba 7, 2023, Israel imewaua wanafunzi wasiopungua 10,490, na kujeruhi wengine 16,700, kulingana na Wizara ya Elimu na Elimu ya Juu ya Palestina.

Zaidi ya walimu 500 wa shule na wasomi wa vyuo vikuu pia wameuawa, na zaidi ya wanafunzi 600,000 wa shule za msingi na sekondari bado wananyimwa haki yao ya kupata elimu, pamoja na zaidi ya wanafunzi 88,000 wa vyuo vikuu.

Vyuo 17 vya elimu ya juu huko Gaza vimeharibiwa kiasi au kuharibiwa kabisa katika milipuko ya mabomu, na thuluthi mbili ya shule za Gaza zikilengwa huku zikitumiwa kama makazi ya watu waliokimbia makazi yao.

Wakati huo huo, katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu, hali ya wasiwasi ya uvamizi inazidi kuwa kubwa, na kulazimisha taasisi 34 za elimu ya juu kuzingatia masomo ya umbali kwa miezi kutokana na kuongezeka kwa ukiukwaji, vikwazo zaidi dhidi ya uhamiaji na ghasia za walowezi.

Wanafunzi na wasomi wa Kipalestina wanalengwa mara kwa mara na jeshi la Israeli, iwe Gaza, Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu, Jerusalem Mashariki au kambi za wakimbizi.

Uanaharakati wao unaharamishwa, haki yao ya kutembea imezuiwa, vyuo vikuu vyao vinavamiwa, na pia kunyimwa kwa uhuru wao wa masomo.

Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Birzeit katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa waandamana kuunga mkono Gaza mnamo Juni 10, 2024. /Picha: (Zain JAAFAR / AFP).

Zaidi ya wanafunzi 2,500 kutoka Chuo Kikuu cha Birzeit katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu wamefungwa tangu 1982, huku zaidi ya 140 bado wanaendelea kufungwa.

Zaidi ya wanafunzi 70 kati ya hao walizuiliwa baada ya Oktoba 7, 2023, wakiwemo wanafunzi sita wa kike, na wasomi wanne wa chuo kikuu na wafanyikazi. Wengi wanasalia chini ya kizuizi cha kiutawala, wamezuiliwa kwa muda usiojulikana bila kufunguliwa mashtaka.

Kushirikishwa na ujinga

Hii inatuleta kwenye swali muhimu sana: kwa nini elimu ya Palestina inalengwa kwa utaratibu?

Linapokuja suala la kudumisha hali ya ukoloni wa walowezi wa Kiisraeli huko Palestina, ujinga hutumika kama mshirika mkubwa, unaowezesha kuanzishwa kwa masimulizi makubwa. Elimu kwa upande mwingine inaibuka kama nguzo kuu ya upinzani, uthabiti, uwezeshaji wa kiasili na ukombozi.

Uharibifu unaoendelea wa mfumo wa elimu wa Gaza unaonyesha uzito wa shambulio hili lililokusudiwa, ambalo wasomi sasa wanalitaja kama "mauaji ya kielimu." Neno hili lililoanzishwa na profesa wa Oxford Karma Nabulsi wakati wa shambulio la Israeli la 2008-2009 huko Gaza linalojumuisha uharibifu wa kimakusudi wa elimu huko Palestina.

Mkakati huu, sehemu ya sera pana ya ukoloni, unalenga sio tu kukandamiza miundombinu ya kimaumbile ya kujifunza, bali pia kuangamiza ukuaji wa kiakili wa watu.

Elimu inashambuliwa kimfumo kwa sababu inawakilisha aina ya upinzani kwa Wapalestina. Ni njia ambayo Wapalestina wanaweza kutoa changamoto kwa masimulizi makubwa ya kikoloni, kuhifadhi historia na utambulisho wao, na kuwawezesha vizazi vijavyo.

Kufufuka tena

Licha ya mashambulizi ya kimfumo kwenye mfumo wao wa elimu, Wapalestina wanasalia na msimamo katika harakati zao za kutafuta elimu.

Wakati wa intifadha ya kwanza mwaka 1988, Chuo Kikuu cha Birzeit na taasisi nyingine zilipofungwa chini ya amri za kijeshi, Wapalestina walipata njia mbadala za kuendelea na elimu yao. Masomo ya siri yalifanyika katika nyumba za wanafunzi na wasomi, vituo vya jamii, na mahali pengine.

Kwa hivyo kwa Wapalestina, kuna simulizi mbili linapokuja suala la elimu. Kwa upande mmoja, ni kitendo cha kupinga. Sio tu kupigania uhuru wa kielimu, lakini mapambano ya kuishi.

Wapalestina wanaendelea kuamini katika nguvu inayosababishwa na elimu. Ustahimilivu wao, ambao mara nyingi hujulikana kama 'Sumud', ndio unaowafanya kusonga mbele. Elimu ni msingi wa utambulisho wa Wapalestina, ambao unafungamana sana na harakati za kujitawala.

Kwa upande mwingine, elimu imekuwa ikivamiwa na wakaliaji wa mabavu ili kuwatiisha na kuwadhibiti Wapalestina. Hii inaimarisha utawala wa uvamizi wa Israeli na kuendeleza ajenda yake ya kikoloni.

Leo, shambulio la Israeli dhidi ya elimu limekuwa zaidi ya uharibifu wa jengo la shule. Inashambulia ukuaji wa akili, urithi wa kitamaduni, na uongozi wa siku zijazo.

Huko Gaza, uharibifu wa shule na taasisi za elimu ya juu, hauwakilishi tu upotezaji wa majengo lakini kufutwa kwa miongo kadhaa ya maendeleo. Kuua waelimishaji na wasomi kunaonyesha jinsi shambulio hili la elimu linavyotekelezwa.

Uvamizi huo haulengi maisha ya Wapalestina pekee, bali pia unalenga kusambaratisha mustakabali wake kwa kuwanyamazisha wale wanaoweza kuongoza njia.

Hata hivyo, mbele ya ukatili huo, watu wa Palestina wanaendelea kunawiri, kama kuzaliwa upya.

Wakati watu wa Palestina wanaendelea kutetea haki zao, ni muhimu kwamba jumuiya ya kimataifa iunge mkono juhudi zao, kuongeza sauti zao, na kutaka Israeli kuwajibishwa kwa kwa uhalifu wa kivita unaofanywa dhidi yao. Azimio la Wapalestina linaonyesha dhamira isiyoyumba ya sio tu kuishi, lakini kustawi kupitia elimu.

Mwandishi: Sundos Hammad ndiye mratibu wa Kampeni ya Haki ya Elimu katika Chuo Kikuu cha Birzeit katika Palestina inayokaliwa kwa mabavu, jukumu ambalo ameshikilia kwa zaidi ya miaka kumi na miwili. Mtetezi aliyejitolea wa haki za binadamu, ana Shahada ya Uzamili katika Masomo ya Kimataifa na amejitolea sana kwa haki ya kijamii na uhuru wa kitaaluma, haswa katika muktadha wa ukoloni wa Israeli.

Kanusho: Maoni yaliyotolewa na mwandishi hayawakilishi lazima maoni, mitazamo na sera za uhariri za TRT Afrika.

TRT World