Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza James Cleverly alisema siku ya Jumamosi alizungumza na serikali ya Israel kuhusu wajibu wake wa kuchukua hatua kwa mujibu wa sheria za kimataifa na kuhifadhi maisha ya raia huko Gaza, na kwa jeshi lake kuonyesha kujizuia.
"Nimezungumza moja kwa moja na Serikali ya Israel, kuhusu wajibu wao wa kuheshimu sheria za kimataifa na umuhimu wa kuhifadhi maisha ya raia huko Gaza," Cleverly aliuambia Mkutano wa Amani wa Cairo ulioandaliwa na Misri.
"Licha ya mazingira magumu sana, nimetoa wito wa nidhamu na weledi na kujizuia kutoka kwa jeshi la Israel."
Wanajeshi wa Israel wamekusanyika kwenye mpaka wa Gaza kabla ya uvamizi wa ardhini unaotarajiwa ambao maafisa wameahidi utaanza "hivi karibuni".
Maelfu ya askari
Waziri wa Ulinzi Yoav Gallant amewataka wanajeshi "kujipanga, kuwa tayari" kwa uvamizi. Israel imekusanya makumi ya maelfu ya wanajeshi kwenye mpaka.
Israel imeapa kuiangamiza Hamas baada ya kundi la wanamgambo wa Kiislamu kufanya shambulio baya zaidi kuwahi kutokea katika historia ya nchi hiyo tarehe 7 Oktoba.
Mashambulio kamili ya ardhi ya Israel yana hatari nyingi, ikiwa ni pamoja na mateka zaidi ya 200 wa liotekwa na Hamas wakati wa uvamizi wao na ambao hatima yao imegubikwa na sintofahamu.
Huko Gaza, ndege za Israel ziliendelea na kampeni ya mashambulizi ya mara kwa mara, huku jeshi likisema lilishambulia zaidi ya shabaha 100 za Hamas kwa usiku mmoja.
Takriban nusu ya wakaazi wa Gaza wameyakimbia makazi yao, kulingana na Umoja wa Mataifa.
Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi wa Kipalestina lilisema Jumamosi kwamba wafanyakazi 17 wamethibitishwa kuuawa katika vita hivyo, na kuonya kwamba idadi halisi "huenda ikawa kubwa".