Na Amir Zia
China inasonga mbeele barani Afrika. Mapema mwezi huu, Beijing ilifanaya mkutano mkubwa zaidi wa kidiplomasia kuwahi kufanyika katika miaka ya hivi karibuni na kuhitimishwa kwa Kongamano la tisa la Ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC).
Kupitia tukio hili kubwa, China na washirika wake wa Afrika walitangaza ujumbe wa "hatma ya pamoja" na "uboreshaji jumuishi".
Viongozi wakuu wa zaidi ya nchi 50 za Afrika, au wawakilishi wao, walihudhuria mkutano huo ambapo Beijing iliahidi kufadhili miradi ya maendeleo barani Afrika yenye thamani ya dola bilioni 50.7 za Marekani.
Ukubwa na ujumbe wa tukio hilo ulionekana kuwa mkubwa na mkubwa zaidi kuliko mikutano ya kilele ya FOCAC iliyopita, na kuibua hisia katika kambi ya Magharibi inayoongozwa na Marekani, ambayo inashindana na China kwa ushawishi katika bara la Afrika.
Hata hivyo, Wachina wanaonekana kuwa wako mbele katika mchezo wa kujenga uhusiano na kupanua biashara na uwekezaji na nchi za Afrika ikilinganishwa na mataifa mengine yote yanayoshindana.
Hii inaonekana katika idadi ya biashara, uwekezaji na madeni ambapo China inaipita Marekani, nchi inayoongoza kwa uchumi duniani. Kwa mfano, China imesalia mshirika mkubwa zaidi wa kibiashara wa Afrika kwa miaka 15 mfululizo. Mnamo 2023, biashara kati ya China na Afrika ilifikia dola bilioni 282.
Mauzo makuu ya China barani Afrika ni pamoja na magari mapya ya nishati, betri za lithiamu na bidhaa za 'photovoltaic' nazo ni bidhaa zinzotumiwa kuzalisha nishati. Nayo China inanunua madini, mboga, matunda na maua.
Kwa upande mwingine, biashara ya Amerika na Afrika ilifikia karibu dola bilioni 68 mnamo 2023. Mauzo ya Marekani kwa nchi za Afrika ni pamoja na ndege, bidhaa za petroli, magari na gesi asilia, huku uagizaji kutoka nje ukijumuisha mafuta ya petroli, madini ya thamani, vito, fedha na nguo.
Kivutio cha pesa
China pia ni mkopeshaji mkubwa zaidi kwa Afrika. Kulingana na utafiti wa Chuo Kikuu cha Boston, China ilikopesha zaidi ya dola bilioni 182 kwa nchi za Afrika kati ya 2000-23, ikisisitiza ukweli kwamba tangu kuanzishwa kwa FOCAC, uhusiano wa kiuchumi wa Beijing na Afrika umeongezeka kwa kiasi kikubwa.
Hata hivyo, kufuatia mlipuko wa janga la Covid-19 mwaka 2019, mtiririko wa fedha za China kwa Afrika ulipungua kwa kasi ikilinganishwa na miaka ya awali ya mradi wa miundombinu wa kimataifa wa China, Mpango wa Belt and Road Initiative (BRI) uliozinduliwa mwaka 2013.
Katika miaka ya mwanzo ya BRI, mikopo ya China kwa Afrika ilikuwa mara kwa mara zaidi ya dola bilioni 10 kila mwaka.
Lakini baada ya kupunguzwa kwa mkopo kwa miaka kadhaa iliyopita, mnamo 2023, kumekuwa na ongezeko la mikopo ya China kwa Afrika hadi kufikia dola bilioni 4.61.
Kwa upande wake, Washington ilifadhili ruzuku 15 za kuandaa miradi kupitia Wakala wake wa Biashara na Maendeleo. Ruzuku hizi zililenga kusaidia karibu dola bilioni 3.4 katika miradi ya ufadhili wa miundombinu kote barani Afrika, ikisisitiza kwamba Wamarekani wamekuwa nyuma katika nyanja hii, ikilinganishwa na Uchina.
Utawala wa Biden pia uliandaa Mkutano wa Viongozi wa Marekani-Afrika mnamo Desemba 2022 - mkutano wa pili wa aina hiyo baada ya pengo la miaka minane. Mkutano huu uliokuwa ukisubiriwa kwa muda mrefu ulihudhuriwa na viongozi kutoka nchi 49 za Afrika.
Hata hivyo, China inaongoza kidiplomasia barani Afrika dhidi ya kambi ya Magharibi inayoongozwa na Marekani kwa sababu kadhaa, ikiwa ni pamoja na ukweli kwamba Beijing ina historia ya kuunga mkono harakati za ukombozi wa Afrika zinazopigana na utawala wa kikoloni tangu mapinduzi ya kikomunisti ya China mwaka 1949.
Tangu mwishoni mwa miaka ya 1990, China imeongeza kwa kasi shughuli za biashara na uwekezaji barani Afrika, na kufikia kilele cha mkutano wa kwanza wa FOCAC mwaka 2000.
Kwa kuzinduliwa kwa BRI mwaka 2013, shughuli hizi zilipata nguvu zaidi licha ya madai ya Magharibi kwamba Beijing inatumia mtego wa madeni kupata mali za mataifa yanayokopa.
Uchina haina shida kujenga uhusiano na nchi za kidemokrasia, kama ilivyo na zile zilizo chini ya utawala wa kidikteta. Beijing haina tatizo kufanya makubaliano na nchi zinazoonekana kuwa karibu na Marekani vile vile haina tatizo kushirikiana na zile zenye uhusiano wa karibu na Moscow.
Wachina hawawahi kuwauliza washirika wake wa biashara na uwekezaji kuunga mkono Beijing katika mzozo wowote kwenye kongamano lolote la kimataifa, hata la Umoja wa Mataifa. Hii inafanya iwe rahisi kwa mataifa yanayoendelea kukabiliana na China.
Kinyume chake, kambi inayoongozwa na Marekani inasalia na nia ya kupeleka mfumo wake wa demokrasia yake, njia ya utawala na fikra ya haki za binadamu duniani kote, hasa katika mataifa yanayoendelea.
Katika Mkutano wa pili wa Viongozi wa Marekani na Afrika, kwa mfano, kuimarisha demokrasia na haki za binadamu kulitumika kama moja ya mada kuu za mkutano huo.
Kwa waliberali, ahadi hii ya Marekani kwa demokrasia na haki za binadamu inasalia kuwa maadili ambayo lazima yatukuzwe na kuthaminiwa.
Hata hivyo, wale wanaosimama upande wa pili wa mgawanyiko huo wanaona kama uingiliaji wa kizembe katika masuala ya mataifa mengine na nchi za Magharibi bila kuzingatia masharti ya lengo, ikiwa ni pamoja na njia ya uzalishaji na kiwango cha maendeleo ya kijamii na kiuchumi ya nchi zinazoendelea.
Wakosoaji hawa pia wanaashiria migawanyiko na migongano ya sera ya nje ya Marekani, ambayo inapuuza kwa urahisi maadili haya wakati inashughulika na tawala teule za nchi zenye utajiri wa mafuta au zile ambazo Washington ina masilahi ya kimkakati.
Vile vile wamekosoa wa sera za nchi za magharibi za kutumia masuala ya demokrasia na haki za binadamu kama kigezo, wakismea kuwa katika jamii zinazoongozwa kikabila , au kifalme, demokrasia na utawala wa mtindo wa Kimagharibi huleta matatizo zaidi kuliko suluhu.
Na kwa hakika, vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu kwa muda mrefu na vya sasa katika nchi nyingi za Asia na Afrika vinasalia kuwa ushuhuda wa mtazamo huu mbovu wa Magharibi.
Mbinu ya mashariki
Katika miezi ya hivi karibuni, nchi nyingi za Kiafrika ambazo zinakataa kuilaani Moscow juu ya vita na Ukraine zimekosoa waziwazi jukumu la Washington katika mzozo huo.
Mtazamo wa China katika kushughulika na nchi zinazoendelea ni kinyume na ule wa Washington na washirika wake, kwani kujenga uhusiano na Beijing kunakuja bila uzito woyote wa kiitikadi au kisiasa.
Beijing, kwa upande wake, pia imejaribu kuweka sera yake kuwa chanya katika toleo la hivi karibuni la FOCAC, ikilenga katika uboreshaji jumuishaji, ukuaji wa siku zijazo, nishati ya kijani, ukuaji wa viwanda, maendeleo ya kilimo, usalama na BRI ambayo inalenga kuunganisha mabara kadhaa na China kupitia miundombinu.
Katika hotuba yake kuu katika mkutano huo, Rais Xi Jinping alitoa maelezo ya haraka juu ya mtazamo wa Magharibi wa mageuzi ya kisasa, akisema kwamba "imesababisha mateso makubwa kwa nchi zinazoendelea".
Wakati akitoa wito wa kusahihisha "ukosefu wa haki wa kihistoria" dhidi ya Afrika, hotuba yake iliyosalia ililenga zaidi malengo ya pamoja ya maendeleo na kuanzisha "wimbi la kisasa katika Kusini mwa Ulimwengu".
Hii inaangazia sera iliyobuniwa kwa uangalifu ya Beijing ya subira ya kimkakati na kutenda kwa hekima ambayo inaiwezesha China kuzingatia kupanua wigo wake wa uchumi wa kimataifa kwa kuzuia migogoro hata baada ya uchochezi.
Mbinu hii hurahisisha maisha kwa viongozi hao wa Kiafrika, pamoja na wengine wengi katika Asia na Amerika Kusini, ambao wanataka kudumisha uhusiano mzuri na Beijing na Washington.
Ushindani wa enzi ya Vita Baridi, wakati Marekani na Umoja wa Kisovieti wa zamani zilipigana vita vya uwakilishi kote ulimwenguni, ikiwa ni pamoja na Afrika, haufai mataifa yoyote yanayoendelea.
China pia inatumia mkakati wake wa kuhamishia teknolojia ya kisasa kwa mataifa yanayoendelea, ambayo ilikuwa moja ya mada katika mkutano wa kilele wa FOCAC.
Haishangazi nchi nyingi zinazoendelea zinaiona China kuwa inawasilisha muundo mbadala wa maendeleo unaoashiria utulivu na mwendelezo.
Hii inasimama kinyume na kambi ya Magharibi inayoongozwa na Marekani, ambapo demokrasia yenye kelele na machafuko, pamoja na uzito wake wa kiitikadi, zinatatiza hata kufanya maamuzi kwa wakati.
Hata hivyo, njia bora zaidi kwa nchi za Afrika, pamoja na nchi nyingi za Asia na Amerika Kusini, ni kusawazisha uhusiano wao na Marekani na China.
Mataifa hayo mawili makubwa yanaweza kuchukua jukumu muhimu katika kusaidia nchi zinazoendelea kuwatoa watu wake kutoka kwenye mtego wa umaskini na kuharakisha maendeleo yao, maendeleo ya viwanda na juhudi za kisasa.
Lakini fikra ya " lazima uwe pamoja nasi au uchague kuwa pamoja nao" ni hatari kwa amani na maendeleo.
Kanusho: Maoni yaliyotolewa na mwandishi hayawakilishi lazima maoni, mitazamo na sera za uhariri za TRT Afrika.