Na
Nilosree Biswas
Alama ya matumaini. Hivyo ndivyo wengi nchini India wanavyoona baada ya kufutiliwa kwa tamasha la filamu la Israeli nchini humo. Tukio hilo lilikuwa lifanyike katika Jumba la Makumbusho la Kitaifa la Sinema ya Kihindi la Mumbai mapema mwezi huu, lakini lilifutililiwa mbali na Shirika la Kitaifa la Maendeleo ya Filamu la India (NFDC) baada ya kupata shinikizo kutoka kwa wananchi.
Taarifa ya pamoja ilitolewa na zaidi ya nyota 1,000 wa filamu, wakurugenzi, wanaharakati na raia ambao walipinga kuandaliwa kwa Tamasha la Filamu la Israeli, kwani mauaji ya halaiki huko Gaza yameendelea sasa kwa miezi 11, huku 40,000 wakiuawa - ikiwa ni pamoja na zaidi ya watoto 15,000.
Waliotia saini ni pamoja na waigizaji wa Kihindi Nasiruddin Shah na Ratna Pathak Shah, mtayarishaji filamu wa hali halisi Anand Patwardhan, na wakili wa haki za binadamu Mihir Desai.
Katika taarifa hiyo, walisema tukio hilo "linafanyika kwa njia ya aibu wakati dunia nzima inashuhudia uhalifu wa kivita wa Israeli (huko Gaza) ... mauaji ya halaiki yanatokea kwa kweli kabisa, na ulimwengu wote unashuhudia uovu huu wa kinyama, tunatazama kwa hofu kwenye mitandao ya kijamii na vyombo vya habari."
Kwa nini NFDC iliandaa hata tukio kama hilo la kuionyesha Israeli, wakati dunia imegawanyika kuhusu suala la Palestina, huku Wapalestina wakiteseka kwa uhalifu mbaya zaidi wa kivita?
Jibu rahisi zaidi itakuwa kwa sababu ni wakala unaoungwa mkono na serikali. Na kwa kuimarika kwa sasa kwa uhusiano kati ya India na Israeli, tukio kama hili lingeendana na mienendo ya serikali yetu.
Katika miaka ya hivi karibuni, India na Israeli zimekuwa washirika wa kiuchumi wenye nguvu. Wamekuwa wakifanya biashara ya silaha na tangu Oktoba, India imekubali kutuma makumi ya maelfu ya wafanyikazi nchini Israeli ili kuziba uhaba wao wa wafanyikazi.
Lakini uamuzi wa NFDC kuandaa tamasha la filamu la Israeli unakwenda zaidi ya uhusiano wa kiuchumi wa India na Israeli. Ili kuelewa kwa kina, tunahitaji kujifunza zaidi kuhusu utata wa filamu inayoendeshwa na serikali ya India.
Kuangalia siku za nyuma
NFDC na mtangulizi wake Shirika la Fedha la Filamu (FFC) ziliundwa ili kusaidia sinema mbadala ambayo inakosoa jamii, kanuni, na kutenda kama mtoa huduma wa kuonyesha mabadiliko.
Lakini chombo hicho pia kina jukumu la kuendana na siasa za wakati huo, kwa kuangazia mafanikio ya serikali au wakati mwingine kusaidia ujenzi wa taswira ya viongozi wa kisiasa kama Waziri Mkuu wa zamani Indira Gandhi.
Kwa mfano filamu ya 1976, Manthan au The Churning, kuhusu mapinduzi ya viwanda vya maziwa nchini India. Ilionyesha siasa za maendeleo kutoka kwa mtazamo wa kijamaa, kwa kiasi kikubwa kutafakari juu ya mafanikio ya mipango ya serikali.
Kwa Gandhi, filamu ilikuwa fursa ya kukuza sura, sura iliyoboreshwa kwa umma alipositisha hali ya Dharura mwaka wa 1977. Zoezi la kujenga taswira liliendelea wakati Gandhi aliporejea kama waziri mkuu mwaka 1980 na kuidhinisha serikali, kupitia NFDC, kutoa $6.5 milioni kusaidia kufadhili wasifu wa Gandhi wa dola milioni 22, alisema mwanahistoria Rochona Majumdar.
"Nchi ya India haijawahi kulipa kiasi kikubwa kama hicho kwa filamu moja," Majumdar aliongeza katika kitabu chake Art Cinema and India's Forgotten Futures - Film and History in the Postcolony."
Kufadhili Gandhi, filamu ya kimataifa yenye waigizaji wa kimataifa na hisia kali, ilikuwa juhudi ya kutendua baadhi ya uharibifu huo" uliosababishwa na hali ya dharura.
Majumdar aliongeza kuwa "mafanikio makubwa ya filamu katika Tuzo za Academy yalithibitisha msimamo wa serikali ya India kuhusu ufadhili wa filamu, hasa kwa vile NFDC ilipokea theluthi moja ya faida ya kimataifa ya filamu."
Bila kusema, sura za kisiasa zilikuzwa na maamuzi kama haya na NFDC ilifaidika na hilo.
Kwa mtazamo huu, kuandaa tamasha la wikendi la filamu za Israeli si la kushangaza, kwa sababu NFDC mara zote imekuwa ikishikilia mstari wa kisiasa, mara nyingi kwa njia ya hila.
Kinachoshangaza ni msukumo uliokumbana nao kutoka kwa mashirika ya kiraia, kiasi kwamba ilihisi kulazimika kusitisha tamasha hilo.
Hata hivyo India haikuwa daima upande wa Israeli.
India - muungaji mkono wa Palestina wa siku za awali
Hadi ziara ya kihistoria ya Waziri Mkuu Narendra Modi nchini Israeli mwaka 2017, India ilikuwa ikiunga mkono kadhia ya Palestina, kutoka awali na kadhalika kihistoria.
Jawaharlal Nehru, muda mrefu kabla ya kuwa Waziri Mkuu wa kwanza wa India, aliwahi kusema mnamo 1936, "Tatizo la Palestina kimsingi ni la utaifa - watu wanaopigania uhuru dhidi ya udhibiti wa ubeberu na dhulma, sio tatizo la ubaguzi wa rangi na wa kidini."
Mahatma Gandhi, kiongozi wa haki za kiraia, alishikilia maoni yake juu ya Palestina, "Palestina ni ya Waarabu kwa maana sawa kwamba Uingereza ni ya Waingereza na Ufaransa ya Wafaransa."
Mawazo haya yalifungua njia kwa uhusiano wa India na Palestina.
Mapambano ya uhuru wa India dhidi ya ubeberu wa Uingereza yalipoongezeka mwishoni mwa miaka ya 1940, msimamo wake wa kisiasa kuelekea Palestina ulizidi kuimarika.
Wakati wa kujiunga kwa Israeli kwenye Umoja wa Mataifa mnamo 1949, Nehru alipiga kura dhidi ya kugawanywa kwa Palestina na Israeli. Wakati wa enzi ya Indira Gandhi (1966-1977).
Aliendelea na msimamo wa mshikamano na alikuwa kiongozi wa kwanza wa serikali kuitambua Jumuiya ya Ukombozi wa Palestina (PLO), mnamo 1974. Pia aligeuza ofisi ya PLO kuwa ubalozi huko New Delhi na akakabidhi vifaa vyote vya kidiplomasia ambavyo ubalozi wowote ungekuwa nao.
Kiongozi wa PLO Yaser Arafat alitembelea India zaidi ya mara moja wakati wa utawala wa Indira Gandhi. Arafat mwenye tabasamu akiwa na kishali chenye rangi nyeusi na nyeupe kwenye kola yake na waziri mkuu akiwa amevalia sari zake za kifahari zinazoonyeshwa kwenye vyombo vya habari vya kitaifa kila viongozi hao walipokutana.
Mnamo 1981, India ilitoa muhuri wa ukumbusho wa rupia moja na udhihiri mdogo wa bendera za India na Palestina. Mnamo 1983, mwaka mmoja kabla ya Gandhi kuuawa, India iliandaa mkutano wa kilele wa 'Non-Aligned Movement' ambapo alithibitisha uungaji mkono wa Palestina.
Msimamo wa Gandhi kuelekea Palestina ulionekena vyema kama sera ya kigeni, lakini pia ulionyesha mwendelezo wa mawazo ya Nehru, ya kijamaa.
Mwendelezo huu wa uungwaji mkono wa Wapalestina unaweza kuonekana leo miongoni mwa wabunge wachache wa India. Wiki iliyopita, wajumbe kutoka Istanbul waliwatembelea kwa matumaini ya kuhimiza serikali ya Modi kubadili msimamo wake kuhusu uvamizi wa Israeli.
Rafiki wa Israeli
Urithi wa India wa sera zinazounga mkono Waarabu ulibadilika baada ya kuanzisha uhusiano wa kidiplomasia na Israeli mnamo 1992, kwa kufungua ubalozi huko Tel Aviv.
Wakati huo, serikali ya Waziri Mkuu Narasimha Rao ilikuza uhusiano huu wa nchi mbili kutokana na wasiwasi wa pamoja kuhusu vitisho vya usalama, ugaidi na ajenda za kawaida kama vile elimu na utalii.
Mwaka huo huo itikadi ya utaifa inayokua ya mrengo mkali wa kulia nyumbani ingeweza kuona ushindi wake wa kwanza, wakati mnamo Desemba, kundi la watu lilibomoa Msikiti wa kihistoria wa Babri.
Katika muongo uliofuata, uhusiano wa India na Israeli uliimarishwa baada ya hatua ya Israeli ya kusambazia India silaha katika Vita vya Kargil - mzozo mfupi kati ya India na Pakistan ambao ulifanyika kutoka Mei hadi Julai 1999 katika wilaya ya Kargil ya Jammu na Kashmir na kando ya mpaka unaosimamiwa na wanajeshi (LoC).
Baada ya kubomolewa kwa Babri Masjid, sinema maarufu nchini India ilichukua mkondo mkali wa kusilimia hadithi zisizo sahihi za kihistoria kama vile Bombay (1995), Sarfarosh (1999), na Refugee (2000).
NFDC hata hivyo iliendelea na harakati zake za kutafuta sinema yenye makusidio ambayo mwanahistoria Majumdar anaiita kama sinema "nzuri" "ambayo dhamira yake kuu ilikuwa kukuza sura ya Wahindi."
Kupatia kipaumbele faida ya pesa juu ya dhamiri ya kijamii, hata hivyo uzalishaji ulizidi kuwa mdogo, mbali na madhumuni yake ya awali na mabadiliko ya hali ya kisiasa. Kwa hilo India ilikuwa inaanza utandawazi.
Filamu zinazoungwa mkono na shirika hilo, kama vile 27 Down (1974) simulizi ya familia zisizofanya kazi za tabaka la kati, Garam Hawa (1977) hadithi iliyowekwa kwenye msingi wa Ugawaji, na 'Anatarjali Yatra' (1997) inaangalia mazoezi ya Brahminical ya ndoa ya mitala, ubaguzi wa misingi ya tabaka na marufuku ya kuolewa tena kwa wajane - yalipunguzwa kwa hadhira maalum.
Mcheza sinema wa kawaida hata hivyo hakupendezwa na filamu hizi wala hakujali sana kuhifadhi utamaduni huu wa sinema kama chanzo cha ushirikiano wa kina na India "halisi" na tabaka zake tofauti.
Pia, NFDC ilitambua umuhimu wa faida na ilizindua "Sinema za India" katika jaribio la kupata pesa kwa kuunda ufikiaji mpana wa filamu zake za zamani zilizotengenezwa katika miaka ya 1980. Wakati huo nafasi yake ya awali ya kutengeneza sinema inayozingatia jamii ilikuwa haijapewa kipaumbele.
Na mara tu serikali ya BJP yenye uzalendo wa hali ya juu ilipoingia madarakani kwa muhula wa pili mnamo 2019, ilirekebisha mashirika/taasisi zote kuu za filamu za utumishi wa umma nchini, pamoja na NFDC ambayo sasa inafanya kazi kama shirika inayosimamia mashirika mengine.
Baada ya enzi ya "halia ya dharura", sera huria za Indira Gandhi na ruhusa iliopewa kutengeneza sinema huru ambayo inakosoa uanzishwaji huo ilifanya kazi vizuri.
Kwa hakika, kufutwa kwa tamasha la filamu la Israeli ni ushindi mdogo, wakati Bollywood, sekta ya pili ya filamu kwa ukubwa duniani, imekuwa ikifumbia macho kadhia ya Palestina na mauaji ya kimbari yanayoendelea.
Mwandishi, Nilosree Biswas ni mwandishi na mtengenezaji wa filamu ambaye anaandika kuhusu historia, utamaduni, chakula na sinema ya Asia ya Kusini, Asia na diaspora yake.
Kanusho: Maoni yaliyotolewa na mwandishi hayawakilishi lazima maoni, mitazamo na sera za uhariri za TRT Afrika.