Kiongozi wa Hamas amesafiri hadi Misri mnamo Jumatano huku matumaini yakiongezeka kuwa Israel na Hamas huenda wanaelekea kwenye makubaliano mengine ya kusitisha mapigano na kuachiliwa kwa mateka zaidi katika vita vya Gaza.
Haniyeh aliwasili "Katika mji mkuu wa Misri, Cairo ili kufanya mazungumzo na maafisa wa Misri juu ya maendeleo ya uvamizi wa Zionist (Israeli) juu ya Gaza na masuala mengine," kundi hilo lilisema katika taarifa.
Haniyeh pia alitarajiwa kukutana na mkuu wa Upelelezi wa Misri kwa mazungumzo juu ya "kukomesha uvamizi na kuandaa makubaliano ya kuachiliwa kwa wafungwa," chanzo cha karibu na kikundi hicho kiliiambia AFP.
Kwa upande mwingine, taarifa ya chanzo cha Reuters imesema kuwa pande zote zinaangalia ni mateka gani na wafungwa wapi wanaweza kuachiliwa katika mpango wowote wa Gaza.
Israel inasisitiza wanawake na mateka wa kiume walio dhaifu wajumuishwe katika orodha ya watakaoachiliwa, kulingana na chanzo.
Mazungumzo yanazidi kuendelea juu ya kusitisha mapigano na kuachiliwa kwa mateka zaidi walioshikiliwa na Hamas, lakini pande hizo mbili zinaonekana kuwa mbali kufikia maafikiano.
Awali, Qatar, ikiungwa mkono na Misri na Marekani, ilisaidia kujadili makupaliano ya amani ya wiki moja mwezi Novemba ambapo mateka 80 wa Israel waliachiliwa kwa kubadilishana na wafungwa 240 wa Palestina.