Viongozi kadhaa wa dunia wakiwemo Rais wa Marekani Joe Biden, Waziri Mkuu wa Canada Justin Trudeau, Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa, Kansela Olaf Scholz wa Ujerumani, Waziri Mkuu Giorgia Meloni wa Italia na Waziri Mkuu wa Uingereza Rishi Sunak wamezungumza kuhusu vita kati ya Israel na Hamas, wakisisitiza msaada wao kwa Israel na kutoa wito wa kufuata sheria za kibinadamu, ikiwa ni pamoja na ulinzi wa raia.
Aidha, viongozi hao pia walikaribisha kuachiliwa kwa mateka wawili na huku wakitoa wito wa kuachiliwa mara moja kwa mateka wote waliobaki.
Waliahidi ushirikiano wa karibu kusaidia raia wa nchi hizo katika eneo hilo, hasa wale wanaotaka kuondoka Gaza.
Viongozi hao walikaribisha tangazo la misafara ya kwanza ya misaada ya kibinadamu kuwafikia Wapalestina wenye mahitaji huko Gaza na kujitolea kuendelea kuratibu na washirika katika eneo hilo ili kuhakikisha upatikanaji endelevu na salama wa chakula, maji, huduma ya matibabu na msaada mengine inayohitajika kukidhi mahitaji ya kibinadamu.
Pia walisema wataendelea na uratibu wa karibu wa kidiplomasia, pamoja na washirika muhimu katika mkoa huo, kuzuia mzozo kuenea, kuhifadhi utulivu katika Mashariki ya Kati, na kufanya kazi kuelekea suluhisho la kisiasa na amani ya kudumu.