Polisi na wanajeshi wote wenye magari, silaha wametakiwa kwenda gerezani kuimarisha ulinzi. / Picha: Reuters

Magenge yanayolenga kumuondoa Waziri Mkuu wa Haiti Ariel Henry yamekuwa yakivamia mji mkuu wa Port-Au-Prince tangu Alhamisi.

Idadi ya wafungwa isiyojulikana wamekimbia baada ya magenge yaliyojihami kuvamia gereza kuu la mji mkuu wa Haiti Port-Au-Prince Jumamosi jioni, kulingana na ubalozi wa Ufaransa na vyombo vya habari vya eneo hilo.

"Jumamosi hii jioni, majambazi walivamia gereza la kitaifa huko Port-Au-Prince na kuruhusu wafungwa kadhaa kutoroka," ubalozi wa Ufaransa ulisema katika barua iliyotumwa kwa AFP.

"Tukisubiri ufafanuzi wa hali hiyo, ubalozi wa Ufaransa unashauri dhidi ya safari zote katika eneo la mji mkuu wa Port-Au-Prince," ilisema.

Aidha, kupitia ujumbe ulioandikwa kwa lugha ya Creole na kuchapishwa kwenye mitandao ya Kijamii ya jukwaa la X, idara ya polisi ya Taifa la Haiti SNPH - 17 iliwaomba polisi na wanajeshi wote wenye magari, silaha na risasi kwenda gerezani kuimarisha ulinzi.

Kulingana na gazeti la habari la Haiti, "idadi kubwa ya wafungwa walioachiliwa" na magenge yenye silaha ni "wanachama muhimu wa magenge yenye nguvu sana."

Viongozi maarufu wa magenge wakiwemo wale walioshtakiwa kwa mauaji ya 2021 ya rais Jovenel Moise walikuwa miongoni mwa wale waliofungwa gerezani, iliyoko mita mia chache kutoka Ikulu ya Kitaifa, Gazeti la Haiti Le Nouvelliste lilisema.

Haikutoa maelezo yoyote kuhusu idadi au maelezo mafupi ya wafungwa waliotoroka.

Kulingana na gazeti hilo la Le Nouvelliste, gereza hilo lilikuwa "limepelelezwa na washambuliaji tangu Alhamisi kupitia ndege zisizo na rubani", kabla ya kushambuliwa mapema Jumamosi jioni,

Taifa hilo la Karibiani tayari lilikuwa chini ya vurugu za magenge lakini magenge sasa yanadhibiti asilimia 80 ya Port-Au-Prince, na uhalifu mkubwa umefikia viwango vya kuvunja rekodi katika taifa masikini zaidi la ulimwengu wa Magharibi, kulingana na Umoja wa Mataifa.

AFP