Baraza la mpito la Haiti limemtangaza Garry Conille kama Waziri Mkuu wa nchi hiyo/Picha: AFP

Garry Conille ametangazwa kama Waziri Mkuu wa Haiti na Baraza la mpito la nchi hiyo, Rasi wa baraza hilo Edgard Leblanc Fils aksiema siku ya Jumanne.

Conille, ambaye alichaguliwa na wajumbe sita kati ya saba, aliwahi kuwa waziri Mkuu wa nchi hiyo kuanzia Oktoba 2011 mpaka Mei 2012 wakati wa Urais wa Michel Martelly, kwa sasa ndiye Mkurugenzi wa UNICEF kwa kanda ya Marekani ya Kusini na visiwa vya Caribbean.

Mwezi uliopita, Michel Patrick Boisvert alitangazwa kuwa Waziri Mkuu wa mpito baada ya kujiuzulu kwa Ariel Henry mwezi Aprili, hali iliyoibua vurugu kubwa nchini humo. Makundi na magenge mbalimbali yameendeleza vurugu na uporaji wa maeneo muhimu kama magereza, vituo vya polisi, taasisi za serikali toka Februari 29. Vikundi vya kihalifu vinadhibiti sehemu kubwa ya mji mkuu wa Port-au-Prince, wakihusika na mauaji, vitendo vya ubakaji na unyanyasaji.

Uhasama huo ulianza wakati wa kutokuwepo kwa Waziri Mkuu Henry, ambaye alikuwa akizuru Kenya kukamilisha maelezo ya kutumwa kwa maafisa 1,000 wa polisi kuchukua udhibiti wa taifa hilo la Caribbean.

Hakuweza kurejea nchini kutokana na mashambulizi hayo, na uwanja wa ndege katika mji mkuu ulifungwa kwa karibu miezi mitatu.

Ujumbe huo unaoongozwa na Kenya, ambao uliidhinishwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa mnamo Oktoba 2023, unatarajiwa kutumwa hivi karibuni. Rais wa Kenya William Ruto hivi majuzi alikutana na Rais wa Marekani Joe Biden mjini Washington, ambaye aliahidi kuunga mkono ujumbe huo.

Conille alisomea udaktari na afya ya umma na alifanya kazi na jamii masikini huko Haiti, ambapo alisaidia kuratibu juhudi za ujenzi baada ya tetemeko kubwa la ardhi la 2010.

Alifanya kazi kwa miaka kadhaa katika Umoja wa Mataifa kabla ya kuteuliwa kuwa waziri mkuu lakini alijiuzulu chini ya mwaka mmoja baadaye kutokana na kutoelewana na rais na Baraza lake la Mawaziri. Ataliongoza taifa hilo la Caribbean hadi kuandaliwa kwa uchaguzi mkuu mwishoni mwa mwaka ujao.

AA