Raia wa Haiti wakiandamana kwenye mitaa ya  Port-Au-Prince, wakishinikiza  Waziri Mkuu Ariel Henry kundoka madarakani./Picha: Reuters

Maandamano makubwa yamezuka mjini Port-Au-Prince kwa siku tatu mfululizo, kushinikiza kuondolewa kwa Waziri Mkuu Ariel Henry madarakani.

Kwa upande wake, Henry mwenyewe ameomba raia kuwa watulivu.

Raia wamekuwa wakiandamana nchini nzima baada ya Ariel kugoma kujiuzulu February 7, kama alivyoahidi hapo awali.

Februari 7 ni siku ya kipekee katika historia ya nchi hiyo. Mnamo 1986, Dikteta wa zamani Jean-Claude Duvalier alikimbilia Ufaransa, na mnamo 1991, Jean-Bertrand Aristide, rais wa kwanza wa Haiti aliyechaguliwa kidemokrasia, aliapishwa.

"Nadhani sasa wakati umefika kwa sote kuweka vichwa vyetu pamoja kuiokoa Haiti, kufanya mambo kwa njia tofauti katika nchi yetu," Henry alisema bila kutoa ufafanuzi.

Waziri Mkuu Ariel Henry ameomba utulivu katika hotuba kwa taifa mapema Alhamisi. Picha: Reuters

Amewahimiza Wahaiti wasiwachukulie Serikali au Polisi wa kitaifa wa Haiti kama maadui zao.

Wale waliochagua vurugu, uharibifu na kuua watu ili kuchukua madaraka "hawafanyi kazi kwa masilahi ya watu wa Haiti," alisema.

Nchi hiyo ilishindwa kufanya uchaguzi ulipangwa kufanyika 2019 na 2023, na Henry alichukua madaraka kwa uungwaji wa jamii ya kimataifa kufuatia mauaji ya Rais Jovenel Moïse, ya Julai 2021.

Hata hivyo, Henry ameahidi tena kufanya uchaguzi mkuu mara tu masuala ya utovu wa usalama ya Haiti yatakapotatuliwa, akisema kuwa ataendelea kufikia na kufanya kazi na wale wote ambao wanataka nchi iendelee mbele, "kuchukua maamuzi pamoja ambayo yatatusaidia kutoka kwa mgogoro.”

Henry alisema kuwa ataendelea kushinikiza kupelekwa kwa jeshi la polisi la Kenya linaloungwa mkono na Umoja wa mataifa ingawa hatua hiyo kwa sasa imezuiwa na amri ya mahakama.

Mahakama ya Kenya imefanya uamuzi kuwa itakuwa kinyume na katiba kuwapeleka askari wake nje ya nchi isipokuwa kungekuwa na "mpango wa kuafikiana" na serikali mwenyeji.

Mwishoni mwa mwezi Januari, Rais wa Kenya William Ruto aliliambia shirika la habari la Reuters kuwa nchi yake itasonga mbele na mipango ya kutuma maafisa wake kwenye ujumbe wa usalama ulioidhinishwa na Umoja wa Mataifa kwenda Haiti, licha ya uamuzi wa mahakama kupinga kutumwa kwa wanajeshi hao.

AP