Na Ahmad Ibsais
Katika mauaji ya kimbari yanayoendelea Gaza, Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani imethibitisha kile tunachokijua wakati wote - kwamba Israeli imekuwa ikizuia kwa makusudi misaada ya kibinadamu iliyokusudiwa Gaza.
Habari hizo zilithibitishwa na USAID na Ofisi ya Idara ya Idadi ya Watu, Wakimbizi na Uhamiaji ya Wizara ya Mambo ya Nje mwishoni mwa mwezi Aprili.
Hata hivyo, katika hali ya kutatanisha, Waziri wa Mambo ya Nje Antony Blinken alitoa ushahidi mbele ya Bunge la Congress mwezi Mei, akidai kinyume chake—kwamba Israeli haikuzuia misaada inayoungwa mkono na Marekani.
Mkanganyiko huu wa wazi unaonekana kulenga kuepusha sheria muhimu ya Marekani inayoamuru kusitishwa kwa misaada ya kijeshi kwa nchi zinazozuia usaidizi wa kibinadamu.
Kiini cha suala hili ni Kifungu cha 620I cha Sheria ya Usaidizi wa Kigeni, ambayo inakataza msaada wa kijeshi kwa mataifa ambayo yanazuia utoaji wa misaada ya kibinadamu inayofadhiliwa na Marekani.
Sheria hii haijatumika mara chache, lakini ilipaswa kuamilishwa miezi iliyopita wakati wataalam wa USAID na Idara ya Jimbo walipotoa taarifa kuhusu kizuizi cha Israeli.
Kwa mujibu wa risala za ndani za USAID, Israeli sio tu imekataa misafara ya bidhaa muhimu, kama vile chakula, dawa, na vifaa vya usafi, lakini pia imeshambulia wafanyakazi wa misaada, kushambulia hospitali, na kuharibu miundombinu muhimu huko Gaza.
Kuongeza maradufu
Badala ya kutekeleza sheria hiyo, utawala wa Rais wa Marekani Joe Biden umeongeza maradufu msaada wake wa kijeshi kwa Israeli, na kutuma kati ya shehena moja hadi mbili za silaha kila siku tangu kuanza kwa vita dhidi ya Gaza.
Hii ni pamoja na kifurushi cha silaha chenye thamani ya dola bilioni 20 ambacho kiliidhinishwa tu mwezi uliopita, Agosti 2024.
Israeli, nchi iliyopokea msaada mkubwa zaidi wa kijeshi wa Marekani, imetumia silaha hizi katika mashambulizi ambayo yameua zaidi ya Wapalestina 41,000, wengi wao wakiwa raia.
Wataalamu wa Wizara ya Mambo ya Nje, pamoja na maafisa kutoka USAID, wameonya mara kwa mara kwamba hatua za Israeli zinaweza kuzingatiwa kuwa ni kinyume cha sheria chini ya sheria za kimataifa na zinapaswa kusababisha utoaji wa Marekani yenyewe kusitisha msaada wa kijeshi.
Hata hivyo, ushuhuda wa Blinken mbele ya Congress ulipuuza matokeo haya, akidai kwamba Israeli ilikuwa inafuata viwango vya kibinadamu.
Kukanusha huku kwa ukweli sio tu kunalinda Israeli kutokana na uwajibikaji lakini pia kuwezesha kuendelea kwa mashambulizi ya mabomu dhidi ya Gaza na maafa ya kibinadamu yanayozidi kuwa mbaya huko.
Hadi kufikia Machi 2024, zaidi ya malori 930 ya misaada yalisalia kukwama nchini Misri, yasingeweza kuingia Gaza na kutoa chakula cha kuokoa maisha kutokana na ucheleweshaji wa kimakusudi wa Israeli.
Taarifa ya Blinken haikuwa tu suala la uangalizi. Ilikuwa ni hatua ya kimkakati ya kuruhusu silaha hizo kuendela kupelekwa Israeli, huku akifumbia macho maafa ya kibinadamu yanayotokea Gaza.
Licha ya wito wa mara kwa mara kutoka kwa wabunge wa chama cha Democratic na mashirika ya kutetea haki za binadamu kusitisha usafirishaji wa silaha, utawala wa Biden umepuuza ukiukwaji wa wazi wa sheria za Marekani na kimataifa.
Kuhalalisha ushirikiano
Ushirikiano huu unaoendelea unazua swali muhimu: Kwa nini Marekani imeruhusu hili kutokea?
Sababu moja ni muungano wa kina wa kisiasa na kijeshi kati ya nchi hizo mbili, ambao kihistoria umetanguliza usalama wa Israeli kuliko maisha ya Wapalestina.
Maafisa kama Balozi wa Marekani nchini Israeli Jack Lew wameendelea kuamini uhakikisho wa Tel Aviv, licha ya ushahidi mwingi wa kushindwa kwao kuzingatia viwango na hali ya kibinadamu.
Lew hata alipinga wasiwasi wa ndani wa Wizara ya Mambo ya Nje juu ya vikwazo vya Isreali kuzauia kuingiza misaada, akijaribu kuifanya Israeli kama nchi yenye kuzingatia viwango na hali ya kibinadamu na kupuuza uharibifu wa wafanyikazi wa misaada na rasilimali huko Gaza.
Zaidi ya hayo, hoja ya Israeli kwamba vifaa kama vile vifaa vya usafi, taa za jua, na vifaa vya kuondoa chumvi vinaweza kutumiwa tena na Hamas kama nyenzo za "kutumiwa kwa njia zingine" imetumika kuhalalisha vikwazo hivi.
Lakini ucheleweshaji huu ni wa kiholela na unasaidia tu kuongeza mateso ya raia wa Gaza. Kutokuwa tayari kwa serikali ya Marekani kuchukua hatua juu ya matokeo haya kunaonyesha ushirikiano wake mpana katika mfumo ambao unatanguliza utawala wa kijeshi juu ya haki za binadamu.
Zaidi ya kutokubali kwao kufuata sheria za kimataifa za kibinadamu, kuna usaidizi na ushawishi mkubwa katika kusukuma uwongo wa Israeli kuunda uungwaji mkono wa umma kwa mauaji haya ya kimbari.
Kwa mfano, Biden alisema aliona watoto wasio na kichwa baada ya Oktoba 7 (hakuona), wakati wanasiasa wengine wa Marekani wamekuwa wakisambaza madai (yasiyothibitishwa na yaliyokanushwa) ya ubakaji mkubwa.
Hadithi hizi zilitoka kwa serikali ya Israeli ili kuhalalisha mauaji yake ya kimbari, lakini mwishowe zote zilithibitishwa kuwa za uwongo. Hata hivyo Marekani inaendelea kuunga mkono madai hayo bila uthibitisho wowote katika jaribio la kuunda uungaji mkono wa umma kwa Israeli.
Huku hali ya Gaza inavyozidi kuwa mbaya, Marekani lazima ihesabu jukumu lake katika ukatili huu. Sheria iko wazi: nchi inapozuia misaada ya kibinadamu, msaada wa kijeshi wa Marekani lazima ukome.
Lakini badala ya kutekeleza ulinzi huu wa kisheria, Marekani inaendelea kuchochea ghasia.
Udanganyifu wa utawala kuhusu ukweli unaotendeka ili kuepusha athari za kisheria unaonyesha kutojali kwa wazi maisha ya Wapalestina na kudhoofisha zaidi uaminifu wa Marekani kama kiongozi wa kimataifa wa kibinadamu.
Siku ya Jumanne, Biden alizungumza katika Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, hotuba yake ya kwanza huko tangu vita dhidi ya Gaza kuanza.
Katika hotuba yake, Biden alisisitiza tena uwongo wa Israeli kuhusu unyanyasaji mkubwa wa kingono mnamo Oktoba 7 na kuendelea kuhalalisha mauaji ya kimbari yanayoendelea kwa sababu ya mateka wa Israeli waliopotea - kana kwamba Israeli haijawaua mateka hawa wengi, na kukataa mikataba mingi ya kusitisha mapigano.
Biden pia alimuita rais wa Urusi Vladmir Putin kuwa kikwazo cha amani, ingawa rais wa Marekani ndiye anayeendelea kufadhili na kuunga mkono maangamizi makubwa ya Wapalestina.
Ulimwengu unatazama, na historia itakumbuka mahali ambapo Marekani ilisimama wakati huu wa shida.
Ikiwa Biden anataka amani, kama anavyotangaza, lazima aoshe mikono yake iliyochafuliwa na damu na kutoa wito wa kuwekewa vikwazo kamili vya silaha na sheria ya kimataifa kutekelezwa kwa Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanahyu.
Hatutasahau kuunga mkono utawala wa Biden kwa mauaji ya kimbari, na Biden hataweza kamwe kufura historia yake kwa maelfu ya raia wasio na hatia waliouawa kwa kisingizo cha uvamizi wa makazi.
Marekani haiwezi tena kujificha nyuma ya uwongo wa diplomasia. Mfumo wa kisheria upo ili kukomesha aina hii ya ushirikiano, lakini bado haujatumika. Hadi pale serikali ya Marekani itakapokubali na kushughulikia jukumu lake katika mauaji ya kimbari ya Israeli huko Gaza, itaendelea kuwa mshiriki mwenza katika kuangamiza watu wote.
Ulimwengu unatazama, na historia itakumbuka mahali ambapo Marekani ilisimama wakati huu wa shida.
Mwandishi, Ahmad Ibsais ni Mpalestina Mmarekani wa kizazi cha kwanza na mwanafunzi wa sheria ambaye anaandika jarida la State of Siege.
Kanusho: Maoni yaliyotolewa na mwandishi hayawakilishi lazima maoni, mitazamo na sera za uhariri za TRT Afrika.