Al Hayya alimuelezea Sinwar kama shujaa ambaye hakuwa tayari kurudi nyuma./Picha: AFP

Hamas imethibitisha kifo cha kiongozi wao wa kisiasa, Yahya Sinwar, aliyeuwawa na majeshi ya Israeli, huku kikundi hicho kikisisitiza kuwa mateka wa Israeli hawatoachiwa mpaka Israeli isitishe mashambulizi yake na ijiondoe kwenye eneo la Gaza.

"Wale mateka hawatoachiwa kabla hamjaacha kutekeleza machafuko katika eneo la Gaza na kabla hamjajiondoa eneo hilo," afisa wa Hamas Khalil al Hayya alisema siku ya Ijumaa.

Katika taarifa iliyotolewa kwa picha mjongeo, Hamas ilimuelezea Sinwar kama "shujaa aliyefikia daraja la ushahidi, akiendeleza mapambano bila kurudi nyuma".

Taarifa hiyo ilionekana kama majibu kwa picha mjongeo inayomuonesha hatua za mwisho za uhai wa Sinwar, ambapo mtu mmoja anaonekana ameketi kwenye kiti ndani ya jengo lililoharibiwa vibaya huku akiwa amejaa vumbi pamoja na majeraha.

Picha hiyo, pia inamuonesha mtu mmoja akiinua fimbo iliyoko mkononi mwake mbele ya shambulio la Israeli.

Mashambulizi ya Israeli yanaendelea

Hezbollah imekuwa ikiilenga Israeli kwa maroketi toka kuanza kwa vita katika eneo la Gaza.

Israeli imeazimia 'kuisambaratisha Hamas' katika eneo lililozingirwa la Gaza, na kumuua Sinwar. Picha zilizopigwa na majeshi ya Israeli, vilimuonesha mwili wa binadamu, anayehisiwa kuwa ni Sinwar, ukiwa umefukiwa kwenye vufusi huku ukiwa umejaa majeraha.

Katika hotuba yake ya siku ya Alhamisi, Waziri Mkuu wa Israeli, Benjamin Netanyahu alisema kuwa “vita vyetu bado havijaisha".

Huko Israeli, familia za mateka wanaoendelea kushikiliwa mjini Gaza, waitaka serikali ya Israeli kurejea mazungumzo kwa nia ya kuwarejesha nyumbani wapendwa wao, wakisema kuwa wanahofia mpango wa ubadilishanaji wafungwa baada ya mauaji ya Sinwar.

Kuna kama mateka 100 waliobakia Gaza, huku Israeli ikisema kuwa imewaua 30 kati yao.

Siku ya Ijumaa, Netanyahu alikuwa amepanga kufanya kikao maalumu kutafuta namna ya kusitisha mapigano na kubadilishana wafungwa, kulingana na afisa mmoja wa Israeli.

Wawakilishi wa Iran ndani ya Umoja wa Mataif wametoa taarifa yenye kumsifia Sinwar, ikisisitiza kuwa Sinwar alikufa kwenye uwanja wa mapambano sio kwenye kificho.

"Roho ya ujasiri itadhihirika ndani ya Waislamu pale tu watakapomwangalia Sinwar akiwa kwenye uwanja wa vita akiwa amevalia mavazi ya mapambano, akikabiliana na maadui.”

Huko Lebanon, kikundi cha Hezbollah kilitoa taarifa yake mapema Ijumaa kikisema kuwa wapiganaji wake wanatumia mtindo mpya kupambana na Israeli.

Kauli ya Hezbollah ilionekana kumaanisha ndege isiyo na rubani iliyosheheni vilipuzi ambayo ilikwepa mfumo wa ulinzi wa anga wa Israeli wenye tabaka nyingi kwenye kambi ya mafunzo ya kijeshi ndani ya Israeli Jumapili iliyopita, na kuua wanajeshi wanne na kujeruhi wengine kadhaa.

Kundi hilo pia lilitangaza mapema wiki hii kwamba lilirusha aina mpya ya kombora liitwalo Qader 2 kuelekea viunga vya Tel Aviv.

Uvamizi wa Lebanon

Jeshi la Israeli lilisema kuwa litaanzisha kikosi cha ziada cha akiba kaskazini mwa nchi yake ili kusaidia wanajeshi wanaovamia kusini mwa Lebanon.

Hezbollah ilisema wapiganaji wake walikuwa wakifanya kazi kulingana na "mipango iliyoandaliwa mapema" ili kupigana na wanajeshi wanaovamia Israeli katika maeneo kadhaa ya kusini mwa Lebanon.

Pia ilitangaza mashambulizi kadhaa ya makombora na mizinga dhidi ya vikosi vya Israeli vinavyokalia vijiji vya eneo la mpaka wa kusini mwa Lebanon usiku na Ijumaa asubuhi.

Katika kisa kimoja, kundi hilo lilisema lilifyatua makombora mazito dhidi ya wanajeshi wa Israel waliokuwa wakijaribu kuwaondoa waliojeruhiwa katika shambulio la awali. Kundi hilo pia limesema limerusha "raundi kubwa za makombora" kwenye kambi ya kijeshi katika eneo la Golan linalokaliwa na Israeli na eneo la Zvulun kaskazini mwa Haifa.

Mapema wiki hii, naibu kiongozi wa Hezbollah Naim Kassem alionya kwamba kundi hilo litaendelea kulenga maeneo mapana ya Israeli tangu mashambulizi ya kikatili ya Tel Aviv yalipoanza mwaka jana, na kuua zaidi ya Wapalestina 42,000, wengi wao wakiwa raia.

TRT Afrika