Mamlaka za Denmark zimekamilisha uchunguzi wiki hii na kusema kuwa bomba la gesi la Nord Stream liliharibiwa kwa kulipuliwa kama kitendo cha hujuma, lakini hawajawekea lawama nchi yoyote.
Aidha Uswidi nayo imesema kuwa uchunguzi wa awali unaonesha kuwa kitendo cha kulipua bomba hilo kilikuwa ni cha hujuma vilevile.
Hatahivyo maswali yanazidi kuibuka ya ni nani hasa anafaidika na hujuma ya aina hiyo na kwa njia gani.
Wachanganuzi wa kijeshi katika ukanda huo wanasema itakuwa ni vigumu kwa washukiwa kutajwa hadharani ikizingatiwa kuwa hali bado ni tete kati ya Urusi na Ukraine.
“Nina uhakika kuwa Uswidi haitamtaja yeyote. Hawataki kuchapisha chochote kwani labda wanajiuliza iwapo wana nguvu ya kutosha ikitokea aliyeharibu bomba ni Urusi,” anasema Jens Wenzel Kristoffersen, ambaye ni mchanganuzi katika chuo kikuu cha Copenhagen.
“Ripoti ya uchunguzi ikiwekwa hadharani huenda hilo likazua tumbo joto na kuzua hofu ya usalama katika Bahari ya Baltiki, ambayo zamani ilifahamika kama Bahari ya Amani, lakini sasa hivi Uswidi na Finland zinavyokaribia kujiunga na NATO, wanaipa jina bahari ya NATO,” anaeleza TRT World.
Mabomba tatu ya gesi ya Nord Stream kati ya manne yanayosafirisha gesi ya Urusi mpaka Ujerumani yameharibiwa vibaya. Kampuni ya Blueye Robotics majuzi ilionesha uharibifu wa Nord Stream 1 kupitia kanda fupi ya video.
Baadhi ya sehemu za bomba hazionekani nadhani kutokana na mabaki na takataka zilizotokana na uharibifu huo.” Anasema Trond Larsen ambaye ni mfanyakazi wa Blueye Robotics.
“Naweza nikasema angalau mita 60 zimeharibiwa na chuma zimepinda,” anaeleza TRT World.
Kabla uvamizi wa Urusi nchini Ukraine mwezi Februari, Urusi ilikuwa ikisafirisha takriban asilimia 40 ya gesi kwenda ulaya lakini kwa vile sasa Nord Stream imefungwa, usafirishaji umesitishwa na kusababisha ongezeko la gharama ya gesi barani ulaya.
Lakini ni kwani uchunguzi juu ya uharibifu wa Nord Stream haukufanyika kwa kushirikiana?
Denmark, Ujerumani na Uswidi zilifanya uchunguzi kivyao na baadae kukawa na pendekezo la kuunda kikosi-kazi cha pamoja lakini Uswidi ikagoma kukubali. Ofisi ya mwendesha mashtaka wa Uswidi haikujibu TRT walipotaka kujua iwapo wameng’amua washukiwa wowote. Aidha Mkurugenzi mkuu wa Baraza la mataifa ya Bahari ya Baltiki, vilevile aligoma kutoa majibu kwa TRT ya ni kwa nini nchi wanachama palikosekana kikosi-kazi cha pamoja.
“Sababu moja kuu huenda ikawa ni kuepukana na Urusi, ambayo ilisisitiza kuwa sehemu ya kikosi-kazi cha uchunguzi,” anasema Carsten Rasmussen, ambaye ni Brigedia Jenerali mstaafu wa Denmark.
“Hakuna uaminifu kati ya Urusi na mataifa haya tatu ya Magharibi. Wanashuku huenda ni Moscow iliyosababisha hujuma hiyo,” anaeleza TRT.
Aidha inasadikiwa kuwa hakutakuwepo na maendeleo yoyote kuhusu ni nani aliyesababisha hujuma hiyo mpaka pale ambapo mamlaka za Denmark na Uswidi zitakapoweka wazi ripoti za uchunguzi wao.