Blinken atoa onyo baada ya msafara wa wanadiplomasia wa Marekani kupigwa risasi Sudan

Blinken atoa onyo baada ya msafara wa wanadiplomasia wa Marekani kupigwa risasi Sudan

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken anasema hatari yoyote inayoletwa kwa wanadiplomasia wa Marekani haikubaliki
Blinken

Msafara wa kidiplomasia wa Marekani umeshambuliwa nchini Sudan na wanaoshukiwa kuwa wapiganaji wanaohusishwa na kikosi cha kijeshi cha Rapid Support Forces RSF.

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken ameshutumu shambulio hilo kama la kiholela na hatarishi.

Tukio hilo limesababisha Blinken kutoa onyo kali, ambapo aliwapigia simu viongozi wa RSF Jenerali Mohamed Hamdan Dagalo, anayefahamika Zaidi kama Hemedti, na mkuu wa jeshi la Sudan Jenerali Abdel Fattah al-Burhan, kuwakumbusha kuwa hatari yoyote dhidi ya raia wa Marekani haitakubalika.

"Tuna wasiwasi mkubwa juu ya mazingira ya usalama nchini humo," alisema Blinken, katika mkutano na waandishi wa Habari nchini Japan, baada ya kukutana na ujumbe wa mawaziri saba wa mambo ya nje kutoka nchi mbali mbali.

Mapigano nchini Sudan yamesababisha vifo vya watu 185 na kuwajeruhi wengine zaidi ya 1,800 huku pande zote mbili zikidai kupata ushindi katika vita vilivyohusisha mashambulio ya angani na makombora.

Makabiliano yameendelea licha ya wito kutoka kwa Marekani na mataifa mengine kusitishwa vita Pamoja na kushindikana juhudi za Misri na mataifa ya milki za kiarabu kutafuta maafikiano.

TRT Afrika