Mwanamume akipita mbele ya maduka yaliyofungwa kufuatia machafuko na ghasia dhidi ya wahamiaji kote nchini, Manchester, Uingereza, Agosti 7, 2024. /Picha: Reuters

Na

Sunder Katwala

Uingereza imeshuhudia ghasia, vurugu na machafuko kuwahi kutokea baada ya zaidi ya muongo mmoja katika wiki mbili zilizopita.

Makundi yenye misimamo mikali ya mrengo wa kulia, yakichochewa na habari potofu kwamba mhamiaji Mwislamu alihusika na vifo vya kusikitisha vya wasichana watatu wachanga huko Southport, "ilipiza kisasi" kwa kushambulia misikiti, wahamiaji na makabila ya waliyowachache.

Kijana Mkristo aliyezaliwa Uingereza, huko Wales kwa wazazi kutoka Rwanda, ndiye aliyehusika na mauaji hayo.

Taarifa hizo potofu zilisaidia kuzua vurugu, lakini haingewezekana bila ubaguzi uliofichika ambao ulitafuta tu sababu.

Ubaguzi dhidi ya Waislamu

Kwa hivyo Uingereza ina ubaguzi wa kiasi gani? Taarifa ya muda mrefu ni kuwa na mabadiliko chanya kutoka hapo zamani. Hata hivyo chuki dhidi ya Uislamu ina ufikiaji mpana wa kijamii kuliko aina nyingine nyingi za ubaguzi wa rangi na chuki nchini Uingereza leo.

Mnamo mwaka wa 2019, mmoja kati ya watu 20 waliohojiwa na Utafiti wa Maadili ya Ulaya walisema kwamba hawataki kuishi karibu na Mwislamu. Hii inaweza kuonekana kama takwimu ndogo, lakini dhana potofu pana za kawaida zinaweza kufikia theluthi moja au zaidi ya idadi ya watu.

La kutia moyo, kumekuwa na shutuma nyingi za kisiasa na kuchukizwa na umma kwa ghasia hizo. Kura ya maoni kutoka kwa YouGov hivi majuzi iligundua kuwa asilimia 85 ya watu hawakuridhishwa na ghasia hizo. Lakini asilimia 7 ya watu waliohojiwa walikuwa tayari kusema waliridhishwa, huku asilimia 2 walisema waliridhishwa pakubwa.

Utafiti wa kwanza juu ya mitazamo ya umma juu ya ghasia hizo uligundua kulikuwa na maafikiano ya wengi kwamba wanaoendesha machafuko hayo walikuwa majambazi, sehemu ya wafuasi wa siasa kali za mrengo wa kulia na wabaguzi wa rangi.

Hata hivyo, mmoja wa tano wa wale waliohojiwa waliwataja waandamanaji kama watu wenye wasiwasi wa kweli, na robo ya umma waliona kuwa Waislamu ndio wa kulaumiwa kwa machafuko hayo.

Pia inashangaza ni kiasi gani wapinzani na wafuasi wa ghasia wanaishi katika ulimwengu sawia. Asilimia 62 ya asilimia 7 ya watu hao waliamini kwamba matukio ya ghasia na machafuko yalionyesha maoni ya sehemu kubwa ya nchi.

Watu saba kati ya 10 katika kundi hili walisema Waislamu walihusika na machafuko hayo. Hizo ni dalili za msingi wa itikadi kali wa karibu asilimia 3 au asilimia 4 ya idadi ya watu - ambayo bado ingemaanisha kati ya watu milioni moja hadi mbili wanaoshikilia itikadi kali.

Ni idadi kubwa ya kutosha ya wenye itikadi kali kuweza kusababisa hofu ambayo inapita zaidi ya ghasia wanayoeneza.

Serikali imejibu vipi?

Je, serikali inapaswa kujibu vipi? Serikali mpya ya Waziri Mkuu Kier Starmer inarithi faragha iliyoachwa ya kutosuluhishwa kuhusu suala la chuki dhidi ya Uislamu.

Serikali ya mwisho ya kihafidhina ilianza mchakato wa kufafanua nini maana ya Chuki dhidi ya Waislamu mnamo 2019 - lakini iliachana nayo bila ya kuifanyia kazi yoyote.

Mipango ya kuteua mshauri mkuu kufuatilia suala la chuki dhidi ya Waislamu - kuakisi mbinu iliyochukuliwa kuhusiana na chuki dhidi ya Wayahudi - ilikwama pia.

Neno 'Islamophobia', lililoanzishwa mwaka wa 1997 na taasisi ya wasomi ya usawa wa rangi Runnymede Trust, mara nyingi hutumiwa kwa kumaanisha kitu kimoja na mashirika ya kiraia na wanasiasa kama kisawe cha chuki dhidi ya Uislamu.

Lakini wengine wanahisi kwamba kuzingatia imani ("Uislamu") badala ya wafuasi ("Waislamu") kunaweza kuleta sintofahamu kuhusu dhamira ya vitendo hivyo.

Kuhusu Serikali ya Uingereza, ufafanuzi mzuri wa chuki dhidi ya Uislamu unapaswa kukidhi majaribio matatu: inahitaji kukubalika kwa Waislamu wengi wa Uingereza; kueleweka kuwa na uadilifu na kupata haki ya mipaka na wananchi wenzao wengi; na kuwa kweli kivitendo kwa wale wanaofanya kazi katika sekta ya elimu, mahali pa kazi na vikundi vya kiraia kama sehemu ya juhudi za kukabiliana na kila aina ya chuki na ubaguzi kwa njia thabiti.

Watu wengi wangekubali kwamba sio chuki dhidi ya Uislamu kukosoa mawazo ya kiitikadi au mtazamo wa kisiasa; wala kujadili, kwa nia njema, changamoto za utambulisho na ushirikiano katika Uingereza leo.

Pia watakubali kwamba ni ubaguzi kuwabagua Waislamu kwa kuwa Waislamu, kuwawajibisha Waislamu wote kwa matendo ya watu wachache zaidi, au kuwa na mazungumzo ambayo yatasitishwa ikiwa kwa mfano, Mwislamu ataingia chumbani.

Ufafanuzi ambao utafanyiwa kazi ni hatua ya kuanzia tu. Lengo si tu kuongeza ufahamu kuhusu ukubwa wa chuki dhidi ya Uislamu bali pia kufikia hadhira husika kwa ajili ya changamoto mbalimbali za kupunguza chuki.

Changamoto zimebaki

Miongoni mwa changamoto hizi - waathiriwa wa chuki wanahitaji mshikamano na usaidizi ili kuripoti na kushtaki uhalifu wa chuki. Wale walio na misimamo ya kuunga mkono wachangie sera thabiti za kukabiliana na chuki.

Zaidi ya hayo, chuki inahitaji kuzuiwa - kutumia sera thabiti na kufunguliwa mashtaka, na kupitia juhudi za kuondoa itikadi kali pia.

Ghasia hizo zinaonyesha haja ya kuongezeka kwa shinikizo kwenye mitandao ya kijamii, ambayo inashindwa kutambua mpaka kati ya uhuru wa kujieleza na uenezaji wa udhalilishaji wa chuki na vurugu.

Ufunguo wa kupunguza chuki ni kufikia katika sehemu hizo za jamii ya kawaida ambayo ina mashaka zaidi juu ya Waislamu wa Uingereza kuliko vikundi vingine vya waliyowachache. Ubaguzi dhidi ya Uislamu unapungua kwa kiasi kikubwa katika vizazi vingi nchini Uingereza.

Kuna hisia kidogo ya mgawanyiko wa "wao na sisi" - kwa sehemu kubwa kwa sababu vijana wana mawasiliano mazuri zaidi, kutoka wakiwa na umri mdogo.

Mawasiliano ya kijamii yenye maana hujenga ujasiri na uthabiti - lakini huenea kwa njia isiyo sawa katika jamii yetu. Kuna mawasiliano zaidi kati ya vijana katika miji mikubwa kuliko katika miji iliyo umbali wa maili 20 kutoka kwao, maeneo ya mashambani, au nje ya pwani ambako idadi ya watu mara nyingi ni asilimia 95 hadi 98 ya wazungu.

Ili kusaidia juhudi hizi, kila shule inapaswa kuhakikisha kuwa wanafunzi wote wana mawasiliano ya maana na Waislamu - na katika makundi yote ya kikabila, ya kidini na ya kijamii.

Hilo linaweza kufanyika kwa urahisi katika shule, katika miji mingi, lakini linaweza kuhitaji mikakati makini zaidi, ikijumuisha miradi ya kuunganisha shule katika maeneo yenye watu wenye tofauti ndogo.

Ikiwa changamoto ni kubwa miongoni mwa vizazi vikongwe, fikra bunifu inahitajika kuhusu jinsi ya kuiga mafanikio ya mawasiliano yenye maana kati ya wanafunzi kwa njia ambazo zinaweza kuwashirikisha wazazi na mababu pia.

Ili kukabiliana na chuki dhidi ya Waislamu kwa muda mrefu, haiwezi kuwa kazi ya serikali pekee. Ushirikiano mpana wa raia utahitajika ili kupanua mawasiliano ya maana zaidi kwa wale ambao wana uwezekano mdogo wa kuipitia.

Ni kwa kuunda jumuiya zilizo karibu na zilizounganishwa vyema zaidi ndipo tunaweza kuwa sio tu wakali dhidi ya vurugu na chuki, lakini pia wakali kupambana na sababu za kijamii za ubaguzi.

Mwandishi, Sunder Katwala ni mkurugenzi wa British Future, taasisi isiyoegemea upande wowote inayoshughulikia masuala ya utambulisho, uhamiaji na rangi.

Kanusho: Maoni yaliyotolewa na mwandishi hayawakilishi lazima maoni, mitazamo na sera za uhariri za TRT Afrika.

TRT Afrika