Mkurugenzi wa Mawasiliano katika Serikali ya Uturuki, Fahrettin Altun ameandika makala kwenye nakala Die Presse, moja ya magazeti makubwa nchini Austria inayozungumzia miaka 100 ya uhusiano kati ya Uturuki na Austria.
"Tuna kila sababu ya kusherehekea urafiki huu wa karne kwani umeunganisha daraja la kihistora kati ya Uturuki na Austria," ameandika Altun katika makala yenye kichwa cha habari "Urithi wa Karne: Kuhusu uhusiano wa Uturuki na Austria, iliyochapishwa siku ya Jumatatu.
Katika makala hiyo, Altun aliangazia umuhimu wa kihistoria wa makubaliano ya ushirikiano kati ya Uturuki na Austria, akisisitiza kuwa unabeba ishara ya ukaribu mkubwa wa nchi hizo mbili. Katika karne iliyopita, makubaliano hayo yamezidi kuchochea sio uhusiano wa kisiasa tu, lakini umeongeza pia maelewano zaidi kati ya Waturuki na Waustria.
Kupitia uhusiano huu, Uturuki na Austria zimekutana mara kadhaa kwa njia ya ziara na majadiliano ya kimkakati, yenye kuwezesha maamuzi ya pamoja kwenye mambo muhimu mtambuka yahusuyo nchi hizo mbili.
Ushirikiano katika mambo mbalimbali
Katika makala hiyo, Altun ameangazia uwekezaji mkubwa wa Austria nchini Uturuki, hatua inayoifanya Austria kati ya nchi kubwa kiuwekezaji ndani ya Uturuki. Kiwango cha biashara baina ya nchi hizo mbili kinakadiriwa kufikia thamani ya dola bilioni nne, huku Altun akionesha matumaini ya kuvuka bilioni tano kwa kutilia mkazo wa malengo yaliyoainishwa na Rais Recep Tayyip Erdogan.
Mkurugenzi huyo wa Mawasiliano katika Serikali ya Uturuki aligusia pia maendeleo yaliyofikiwa kwenye uhusiano wa kitamaduni, sanaa na utalii, huku akisisitiza ukubwa na upekee wa uhusiano huo duniani.
Kuhusu haki za binadamu na utu, Altun amesisitiza kuwa Uturuki kila wakati, iko tayari kuheshimu tunu hizi, hususani ushiriki wake katika kutafuta suluhu ya mgogoro wa Gaza.
Kulingana na makala hiyo, Uturuki ina nafasi kubwa katika kutafuta ufumbuzi wa mgogoro kati ya Urusi na Ukraine, kwa kutumia uanachama wake wa NATO.
Altun ana imani kuwa uhusiano kati ya Uturuki na Austria utaendelea kuimarika, kwa kuzingatia ushupavu na uhodari wake katika kutafuta amani, utulivu na ushirikiano. Mkurugenzi huyo wa Mawasiliano katika Serikali ya Uturuki, ameonesha matumaini ya kukua kwa ushirikiano huo, kwa zaidi ya miaka 100.