Muungano wa OIC waafikia kwa pamoja kupigana na habari za kupotosha pamoja na chuki dhidi ya waislamu

Fahrettin Altun, ambaye ni Mkurugenzi wa mawasiliano wa Turkiye amesema kuwa kuna uhitaji mkubwa wa kubuni mikakati madhubuti ya kupigana na habari potofu pamoja na chuki inayoelekezewa waumini wa dini ya kiislamu. Altun alisema hayo wakati akihutubia mkutano wa OIC ambapo wamuzi wa pamoja uliafikiwa kupigana na tabia hiyo. Altun aliongeza kuwa wamuzi huo ni muhimu hasa nyakati hizi ambapo mataifa mengi yanapigana na chuki dhidi ya waislamu.

“Tumeafikia kwa pamoja kujenga ushirikiano wa mataifa ya kiislamu kwa lengo la kupigana na uenezaji wa habari potofu,” alisema Altun.

“Kwa pamoja tumekubaliana kuwa panahitajika sana elimu katika ngazi za uanahabari pamoja na mikakati ya kuhakiki habari zinapotolewa sambamba na mfumo madhubuti wa sheria.” Aliongeza Altun.

Kongamano hilo la siku mbili jijini Instanbul lilihudhuriwa na mawaziri na viongozi wengine wa ngazi za juu kutoka mataifa 57 ambapo umuhimu wa ushirikiano katika sekta ya habari ulijadiliwa.

“Tumejadiliana kuhusu hatari inayotokana na watu kueneza habari potofu kuhusu watu, nchi, jamii ya waislamu na makundi mengine madogo ya watu ulimwenguni.” Alisema Altun.

Aidha Altun pia aligusia suala la Palestine na kusema kuwa nchi ambazo ni wanachama wa OIC zitajitahidi kuripoti kuhusu chuki inayoelekezewa watu wa Palestine Mjini Jerusalem kutoka kwa serikali ya Israel.

“Tutaweka wazi masaibu ya Wapalestina na uongo mkubwa unaonezwa na Israel.”

Kongamano la OIC liliafikia kutoa msaada kwa wakimbizi pamoja na nchi zinazohifadhi wakimbizi. Aidha pia nchi wanachama ziliahidi kulaani vikali dhuluma inayoelekezewa watu kutoka Afrika.

OIC iliweka bayana kuwa jamii ya waislamu inalaani vikali vitendo vya vurugu, vita na ugaidi.

“Tumekubaliana pia tunahitaji kituo cha pamoja cha utangazaji na ramani ya mwelekeo huo itaundwa hivi karibuni.” Aliongeza Altun.

Kongamano lifuatalo la OIC litafanyika nchini Azerbaijan kwa mujibu wa Altun.

AA