Shughuli za kupambana na ugaidi nchini Uturuki zinaendelea katika eneo hilo, inasema Wizara ya Ulinzi ya Uturuki. / Picha: AA
Wanajeshi sita wa Uturuki waliuawa na mmoja alijeruhiwa katika shambulio la kigaidi karibu na mpaka wa Kaskazini mwa Iraq, Wizara ya Ulinzi ya taifa hilo ilisema.

Aidha, angalau magaidi saba "waliondolewa" Kaskazini mwa Iraq, Wizara ya Ulinzi ya Uturuki imeongeza katika taarifa yake Jumamosi.

Serikali ya Uturuki hutumia neno "kuondolewa" kuashiria magaidi husika walijisalimisha au waliuawa au kukamatwa.

Ingawa kuhusika kwa magaidi kwenye shambulio la Ijumaa haikubainishwa, lakini kundi la kigaidi la PKK linajulikana kushiriki katika uvamizi katika eneo hilo.

Magaidi wa PKK mara nyingi hujificha katika mpaka wa Kaskazini mwa Iraq ili kupanga mashambulizi ya kigaidi nchini Uturuki.

Shughuli za kupambana na ugaidi nchini Uturuki zinaendelea katika eneo hilo, inasema Wizara ya Ulinzi ya Uturuki kwenye taarifa yake.

"Tunawatakia rehema za Mwenyezi Mungu wafia imani wetu watakatifu waliopoteza maisha, tunatuma rambirambi zetu na kuitakia subra na uvumilivu familia zao, vikosi vya jeshi la Uturuki na taifa letu tukufu," Wizara hiyo ilisema.

Pia ilitaka afueni ya haraka kwa wanajeshi waliojeruhiwa katika tukio hilo, ambalo ilisema "lilituletea maumivu na huzuni kubwa."

Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki Hakan Fidan alitoa salamu za rambirambi kwa familia za wafia imani, na kusisitiza kujitolea kwa Uturuki kupambana na makundi ya kigaidi na ushirika wao katika taarifa aliyoandika katika mtandao wa X.

Aidha, Makamu wa rais wa Uturuki Cevdet Yilmaz alielezea huzuni yake kuhusu tukio hilo katika taarifa kwenye mtandao wa X huku akitoa salamu kwa familia za askari waliouawa na kuwaombea waliojeruhiwa uponyaji wa haraka.

Mkurugenzi wa Mawasiliano Fahrettin Altun pia alitoa salamu za rambirambi na kuwatakia huruma ya Mwenyezi Mungu askari waliouawa.

Spika wa Bunge Numan Kurtulmus naye aliwaombea neema ya Mwenyezi Mungu "wafia imani" wa Kituruki, akizitakia subra na uvumilivu familia zao na wapendwa wao na uponyaji wa haraka kwa askari waliojeruhiwa.

Katika kampeni yake ya ugaidi ya zaidi ya miaka 35 dhidi ya Uturuki, PKK, inayoorodheshwa kama Shirika la kigaidi na Uturuki, Marekani, na EU imepelekea vifo vya zaidi ya watu 40,000, wakiwemo wanawake, na watoto wachanga.

TRT World